Sheikh Naim Qassem: Wapiganaji wa Hizbullah ni fakhari inayotetemesha mihimili ya Uzayuni

Katibu Mkuu wa Hizbullah Sheikh Naim Qassem amewaandika barua wapiganaji wa harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, akiwapongeza kwa mapambano ya kujivunia wanayoyaendeleza katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake.

Barua hiyo yenye tarehe ya jana Jumatano ni ya majibu, ya kiongozi huyo wa Hizbullah kwa barua aliyoandikiwa na wapiganaji hao wa Muqawama wa Lebanon siku ya Jumamosi iliyopita.

“Nyinyi ni fakhari inayotetemesha mihimili ya Uzayuni,” ameeleza Sheikh Qassem katika barua yake hiyo na akafafanua kwa kusema: “nguvu za Muqawama wenu zinaimarisha uthabiti wetu na kufikia ushindi wetu kwa kumshinda adui yetu”.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amepongeza imani ya wanamapambano hao wa Muqawama katika kuikomboa Quds tukufu na ardhi ya Lebanon, akimaanisha azma yao thabiti ya kuukomboa mji huo mtakatifu na maeneo mengine ya Lebanon ambayo yangali yanakaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Aidha, Sheikh Naim Qassem amewahutubu wanamuqawama wa Hizbullah akisema: “nyinyi ni nguvu ya kukabiliana na kiburi na utaghuti”, akibainisha pia jinsi wanamapambano wa Hizbullah “walivyojitosa kwenye kina kirefu cha kukikikabili kifo, na wakawa wangali wanaendelea kupambana.”

Harakati ya Hizbullah imekuwa ikiendeleza Muqawama madhubuti dhidi ya uvamizi na hujuma kali za utawala haramu wa Israel dhidi ya Lebanon ambao tangu Oktoba 2023 hadi sasa umeshapelekea kuuawa shahidi Walebanon 3,360 wakiwemo wanawake na watoto.

Ulipizaji kisasi wa Hizbullah umehusisha mamia ya operesheni za mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani zinazolenga ngome za kijeshi na vituo hasasi vya utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zilizobandikwa jina bandia la Israel.

Mapema jana, harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon ilitangaza kuwa, zaidi ya wanajeshi 100 wa Israel wameangamizwa na wengine zaidi ya 1,000 wamejeruhiwa hadi sasa kutokana na operesheni za ulipizaji kisasi…/