Sheikh aeleza mbinu kuzifanya ‘ndoa za uji’ zidumu

Morogoro. Shinikizo la kusaka uhalali wa ibada ya funga katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuchochea ndoa nyingi zinazofungwa unapokaribia au wakati wa mwezi huo.

Wasiwasi huo unapigiwa msitari na Sheikh wa Mkoa wa Morogoro, Twaha Kilango, kuwa aghalabu ndoa hizo maarufu kama za uji, huwa hazidumu.

Kwa sababu ya uhalisia huo, Sheikh Kilango amesema ni muhimu wafungishaji wa ndoa hizo wajikite zaidi katika kutoa elimu ya sheria za ndoa kwa wanaooana, ili kuepuka zisivunjike haraka.

Sheikh Kilango ameyasema hayo leo, katika mahojiano yake na Mwananchi Digital kuelekea mwezi wa Ramadhani.

Amesema viongozi wa dini wanaotumika kufungisha ndoa katika kipindi hicho wanatakiwa kutoa elimu kwa wanandoa kuhusu sheria za ndoa ili kuepusha ndoa hizo kuvunjika haraka baada ya kuisha kwa Ramadhani.

Amesema vijana wengi wa Kiislamu wamekuwa wakiingia kwenye ndoa hizo, kwa tamaa au kupata kibali cha kuingia kwenye ibada ya funga.

Kwa mujibu wa Sheikh Kilango, wengi hukosa utayari wa fikra, uwezo wa kuhudumia ndoa na hivyo kujikuta wakiingia kwenye migogoro ya ndoa na hatimaye kuvunjika.

“Masheikh tuna nafasi ya kuhoji utayari wa wanandoa tusikimbilie tu kuchukuliwa mbio mbio kwenda kufungisha ndoa wakati ndoa yenyewe unajua wazi inakwenda kudumu kwa mwezi mmoja.

“Hii haitakuwa sawa na haya si maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Ndoa ni jambo la kheri na zito, hivyo halipaswi kuletewa mzaha au majaribio,” amesema.

Amewasihi vijana wasiingie kwenye ndoa kwa kigezo tu cha kuhalalisha funga zao, Mungu anapaswa kuabudiwa nyakati zote.

“Haiwezekani miezi yote unafanya zinaa ukaamua kumrudia Mwenyezi Mungu kwa mwezi mmoja tu, eti ukiamini hiyo ibada ya mwezi mmoja ndio itakutoa kwenye dhambi,” amesema.

Sheikh Kilango amewataka Waislamu wanaotaka kuingia kwenye ndoa kufuata sheria na maamrisho ya Mungu kwa kuwa talaka ni moja ya mambo yanayomchukiza Mungu.

Aziz Msuya, mmoja wa waumini wa Kiislamu amesema ipo haja kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), kuandaa mafunzo kwa Waislamu wanaotaka kuingia kwenye ndoa, yatakayohusisha sheria za ndoa kwa mujibu wa dini, misingi na namna ya kukabiliana na changamoto.

“Hizi ndoa za mwezi mtukufu wa Ramadhani nyingi watu wanafunga kutokana na mashinikizo ya wazazi, marafiki na watu wa karibu, ili wahusika waweze kufunga, kutokana na hilo wanandoa wanakosa mapenzi ya ndani na utayari wa kufuata misingi ya ndoa,” amesema.

Mkazi wa Morogoro, Hashim Idd, anayetarajia kuoa Februari 21, 2025, amesema ameamua kuoa ili mwaka huu afunge Mwezi Mtukufu wa Ramadhani akiwa amekamilika.

“Huyu mchumba ninayetaka kumuoa nimekuwa naye kwenye mahusiano kama miezi sita hivi, sasa Ramadhani inakuja, nitafanyaje wakati siwezi kufanya zinaa wakati wa mfungo na isitoshe sina mtu wa kunipikia futari wala daku, ila pamoja na mambo yote hayo nampenda,” amesema Idd.

Kwa sababu ya kupisha Mwezi wa Ramadhani, Flora Johanes amekuwa na kibarua cha kurudi kwao kila mwezi huo unapofika ili kumpa nafasi mpenzi wake afunge.

“Nimechoka ikifika Ramadhani ananiambia nirudi nyumbani ili yeye afunge, nikimwambia anioe anasema hatufanani dini, sasa mwaka huu nimekubali kubadili dini anioe na Ramadani ikifika tuendelee kuishi wote, wiki ijayo tunafunga ndoa,” amesema.

Shani Mohamed, kungwi na somo anayefunda maharusi wakati wa ndoa, amesema pamoja na kuwafunda wengi, lakini ndoa nyingi zinapitia changamoto baada ya Mwezi Mtukufu kumalizika.

“Mimi kama mama wa Kiislamu wali wangu nawafunda mambo mengi zikiwemo sheria za ndoa, lakini changamoto inakuja pale ambapo muoaji analenga kutafuta mpishi wa futari badala ya mke.

Ameeleza ndoa nyingi za mwezi huo hasa zile za Kiislamu zinafungwa ili kuhalalisha ibada ya funga kwa wahusika na sio kwa mapenzi na kuridhiana.