Shamba la mikarafuu lateketea kwa moto Pemba

Pemba. Shamba la mikarafuu kisiwani Pemba limeteketea kwa moto chanzo kikitajwa ni tanuri lililotumika kuchoma mkaa kwenye shamba hilo.

Tukio hilo limetokea Machi 3, 2025  katika kijiji cha Chanoni Shehia ya Kilindi Wilaya ya Chakechake ambapo mikarafuu  zaidi ya 50 inadaiwa kuteketea kwenye eneo la zaidi ya robo ekari.

Kwa mujibu wa taarifa mkarafuu mmoja unatoa wastani wa kilo 15 za karafuu. Kwa mikarafuu 50 ni takriban kilo 750 za karafuu zenye thamani ya Sh11.2 milioni.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Kaimu Ofisa Mdhamini wa  Shirika la Biashara la Taifa  la Zanzibar (ZSTC),  Khamis Omar Khamis amesema  kuteketea shamba hilo ni hasara kwani zao hilo ni tegemezi kwa biashara.

“Hii ni hasara kubwa, shirika limekuwa linahamasisha  wakulima kulituza na kuliendeleza zao la Taifa lakini inasikitisha kuona tena miti yake inaungua,” amesema.

Amesema shirika limekuwa likitoa miche kipindi cha mvua kuona zao hilo linaendelezwa lakini juhudi hizo zinarejeshwa nyuma kutokana na  watu kutokuwa waangalifu.

Kwa mujibu wa ofisa mdhamini huyo, shirika linaendelea kufuatilia kwa karibu ili kujua chanzo hasa cha moto huo hatua ziweze kuchukuliwa.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wazalishaji wa Karafuu Zanzibar, Abubakar Mohamed Ali amesema   uchomaji wa moto katika mashamba ya mikarafuu unaathiri miti hiyo, hivyo amewataka wakulima kuachana na tabia ya uchomaji wa moto na mkaa katika mashamba hayo.

Akizungumza mmoja wa wamiliki wa mikarafuu hiyo, Mohamed Abdalla Bakar amesema  chanzo cha moto huo hakijajulikana licha ya watoto wake kutaka kuchoma mkaa katika eneo hilo.

“Inavyosemekana kuna watu walikuwa wanachoma moto kwa ajili ya kurina asari,” amesema.

Wakati huohuo Bibi Shamba kutoka  Wizara ya Kilimo  na Umwagiliaji Pemba, Khadija Juma Abdalla amesema  kwa tathmini waliyoifanya ya moto huo, imeonyesha kuwa mikarafuu mingi imekufa kabisa.