‘Shamba boy’ jela miaka 30 kwa kumbaka mtoto wa bosi wake

Arusha. Mahakama ya Rufani imethibitisha adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela, aliyohukumiwa aliyekuwa mfanyakazi wa shambani (shamba boy), Salum Machimu, kwa kosa la kumbaka mtoto wa mwajiri wake aliyekuwa na umri wa miaka 13.

Hii ni rufaa yake ya pili kukwaa kisiki ambapo rufaa ya kwanza ilisikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga iliyotoa hukumu Juni 22, 2022 ambapo alidaiwa Oktoba 21, 2020 katika eneo la Ilembo Msangama, Wilayani Mpanda mkoani Katavi, alimbaka mtoto wa mwajiri wake.

Mahakama ya rufani ilitupilia mbali rufaa hiyo baada ya kuona haina mashiko na adhabu iliyotolewa ilikuwa sahihi, hivyo kujiridhisha upande wa mashitaka umethibitisha kosa hilo bila kuacha shaka yoyote.

Rufaa hiyo ya jinai namba 345/2022 ilikuwa ikisikilizwa na jopo la majaji watatu ambao ni Augustine Mwarija, Lilian Mashaka na Eliezer Feleshi, walitoa hukumu hiyo Machi 28, 2025 katika kikao chake kilichoketi Sumbawanga.

Katika kesi ya msingi, Salum alishitakiwa kwa kosa la ubakaji ambapo ilidaiwa siku ya tukio mwathirika wa tukio hilo na mdogo wake wa kike walitumwa shambani kwao kwenda kutafuta kondoo waliokuwa wamepotea.

Ilidaiwa baada ya kazi hiyo, mwathirika wa tukio hilo ambaye katika kesi hiyo alijulikana kama MK, alirudi katika hali ya huzuni na kilio na alipoulizwa na mama yake, alidai kubakwa na Salum ambaye naye kwa wakati huo hakuwepo, alitumwa kwenda kutafuta kondoo hao ambapo alirejea jioni.

Shahidi wa pili ambaye ni mama wa MK, alidai Salum aliporejea hakumuuliza kuhusu tukio hilo na badala yake mama huyo alimdanganya amsaidie kumpeleka mwathirika hospitali na wakiwa njiani kuelekea hospitali, mrufani alikamatwa, akapelekwa polisi na baadaye kufunguliwa mashtaka.

Alidai MK aliporejea nyumbani akilia, alimkagua na kubaini kuwa kuna damu zilizokuwa zikimtoka miguuni na alipomchunguza zaidi, alimkuta akivuja damu sehemu zake za siri.

Alidai mrufani aliporudi nyumbani, aliona kwamba alikuwa na nia ya kukimbia na hivyo kumzuia kufanya hivyo, ndipo alipomrubuni kwa kutafuta usaidizi wa kumpeleka mwathiriwa hospitali.

Alidai alikubali lakini akiwa njiani, alijaribu kukimbia na alifanikiwa kumkamata na kwa msaada wa watu wengine, alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Mpanda.

MK ambaye alikuwa shahidi wa kwanza alidai wakiwa shambani na mdogo wake, walikutana na mrufani huyo ambaye pia alikuwa akiwatafuta kondoo hao na kuwa wakiendelea kutafuta kondoo hao alihisi mrufani alikuwa na nia ya kumtenganisha na mdogo wake.

Alidai mrufani huyo alipita njia nyingine na kuchukua fimbo na kuanza kumpiga na kumfukuza mdogo wake na baada ya kumfukuza, alimshika yeye (MK) kumvua nguo kisha kumbaka huku akimuonya asipige kelele ambapo pia alimziba mdomo.

MK alifikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, alifanyiwa uchunguzi na shahidi wa nne ambaye ni Paulo Kilenga ambaye alidai MK alikuwa anavuja damu ukeni kutokana na kuingiliwa na kitu butu.

Katika utetezi wake Salum, alidai kukutana na MK shambani na kuwa yeye alikwenda mtoni kuoga na aliporejea nyumbani wakati anakaribia kulala, alipigiwa simu na shahidi wa pili akimtuhumu kumbaka mwanaye.

Alidai aliombwa kusaidia kumpeleka hospitali na wakiwa njiani, baada ya kukodi bajaj ya kupanda, badala ya kwenda hospitali, alipelekwa Kituo cha Polisi Mpanda.

Alidai shitaka dhidi yake ni matokeo ya madai yake ya mshahara wake ambao haujalipwa kwa miezi 12 kati ya miaka mitatu aliyofanya kazi hapo.

Baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili, ilieleza kesi hiyo imethibitishwa bila kuacha shaka yoyote na kueleza kuwa utetezi huo haukuleta shaka yoyote dhidi ya ushahidi wa mashitaka hasa kuhusu madai yake ya kutokulipwa mishahara.

Pia, ilizingatia mwenendo wa mrufani wa kujaribu kutoroka na kuona kwamba mwenendo huo uliunga mkono kesi ya upande wa mashtaka, hivyo kumkuta na hatia na kumhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela.

Rufaa ya kwanza

Katika rufaa ya kwanza, Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga ilitupilia mbali rufaa hiyo ambapo Salum alikuwa na sababu nne ikiwemo kesi kutothibitishwa, kutoitwa mahakamani mdogo wa MK, ushahidi wa shahidi wa nne ulikubaliwa kimakosa na utetezi wake haukuzingatiwa.

Mahakama hiyo iliona kuwa sababu zote nne hazina mashiko na hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo.

Katika rufaa hiyo, Salum alikuwa na sababu tatu ambazo ni Mahakama Kuu ilikosea kisheria katika kuunga mkono hukumu dhidi yake katika kesi ambayo haijathibitishwa pasipo shaka, Mahakama Kuu ilikosea kuunga mkono hukumu dhidi yake huku upande wa mashtaka kwa kushindwa kuwaita mashahidi akiwemo mjumbe yeyote wa mamlaka ya kijiji na mdogo wa MK.

Sababu nyingine ni Mahakama Kuu ilikosea kisheria kwa kushindwa kuona kwamba Mahakama ya Mwanzo imeshindwa kuzingatia utetezi wa mrufani.

Katika rufaa huyo, Salum hakuwa na uwakilishi wa wakili huku mjibu rufaa akiwakilishwa na mawakili watatu wa Serikali, ambapo alipoitwa kutetea rufaa yake, aliiomba Mahakama kuzingatia sababu zake za kukata rufaa, iruhusu rufaa yake na kumwachia huru.

Uamuzi wa majaji

Jaji Mwarija amesema wamezingatia ipasavyo misingi ya mrufani na mawasilisho ya majibu yaliyotolewa na mjibu rufaa.

Amesema kwa kuanza na hoja ya tatu ambayo ni utetezi wa mrufani kutozingatiwa, wanakubalina na hoja ya wakili wa Serikali kuwa msingi huo hauna mashiko kwani katika ukurasa wa 40 hadi 41 wa kumbukumbu za rufaa hiyo mahakama ya mwanzo ilizingatia utetezi wa mrufani kwamba hakuwa katika eneo la uhalifu wakati huo.

Amesema pia ilizingatia utetezi kwamba kesi hiyo ilitungwa kwa sababu ya chuki iliyokuwepo kati ya mrufani na shahidi wa pili kuhusu madai ya mishahara yake aliyodai kutolipwa na mwajiri wake, hivyo kutupilia mbali sababu hiyo.

Kuhusu sababu ya kwanza na pili, Jaji Mwarija amesema wanakubaliana na hoja ya mawakili wa Serikali aliyesema kwamba hazina mashiko na kuwa kanuni ya msingi kuwa ushahidi wa kweli katika kesi za ubakaji lazima utoke kwa mwathirika wa tukio hilo.

“Katika kesi hii, ushahidi wa mwathiriwa (shahidi wa kwanza) ulipatikana na mahakama ya mwanzo kuwa wa kuaminika na mahakama ya kwanza ya rufaa ilikubaliana na uamuzi hii,” amesema.

Ameongeza: “Tena kutokana na ushahidi wa shahidi wa kwanza ambao kama ulivyopatikana hapo juu, ulikuwa wa kuaminika, ulithibitisha kwamba kosa hilo lilifanywa na mrufani ambaye alikuwa anafahamika sana kwake kabla ya tarehe ya tukio kwa sababu alikuwa mfanyakazi wa mama yake.”

Jaji Mwarija amesema kitendo cha mrufani kujaribu kutoroka akiwa nyumbani na wakiwa njiani kwenda hospitali, kilikuwa kitendo kisichoendana na kutokuwa na hatia na kuwa mwenendo huo uliunga mkono ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili kuwa alitenda kosa hilo.

Jaji Mwarija alihitimisha kuwa kwa sababu hizo wanaona rufaa haina mashiko na kuitupilia mbali ambapo katika hukumu hiyo, nakala yake inapatikana katika mtandao wa Mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *