
Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amewasisitiza walezi wa vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalumu mkoani Morogoro kuwalea watoto hao kwa misingi yenye maadili mema na yanayompendeza Mungu ili kuwa na kizazi bora cha baadaye.
Shaka amesema hayo wakati akikabidhi zawadi za Idd, kwa watoto wa vituo vinne vya kulelea watoto wenye mahitaji maalumu vya mkoani Morogoro akimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima ikiwa ni mwendelezo wa sherehe za Idd zawadi ambazo zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na kusisitiza kuwa maadili ndiyo nguzo kuu ya kudumisha amani na utulivu hapa nchini.
Mkuu huyo wa wilaya amesema, ni jukumu la walimu na walezi kuwalea watoto hao katika maadili mema nakwambia watoto hao wanahitaji malezi bora kama watoto wengine wa nchi hii, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya mazingira yao hususan ya shule na vituo vya malezi.
“Endeleeni kuwalea watoto hawa kwa misingi inayompendeza Mwenyezi Mungu ili tuwe na kizazi bora cha baadaye, wapate elimu itakayowawezesha kujitegemea kiuchumi kwa siku za usoni,” amesisitiza Shaka.
Aidha, Shaka ameihimiza jamii kutambua kuwa jukumu la kuwalea watoto yatima, wenye mahitaji maalumu na wanaotoka katika mazingira hatarishi si jukumu la walezi wa vituo hivyo pekee au la Serikali, bali ni la jamii nzima. Hivyo ameiomba jamii kuwakumbuka watoto hao hasa katika kipindi hiki cha sikukuu.
“Sikukuu hii ya Idd inasheherekewa kwa siku mbili, yaani Idd mosi na Idd pili, pia hivi karibuni tutakuwa na sherehe za sikukuu ya Pasaka nazo watoto wanapaswa kufurahia. Niiombe jamii isiwasahau watoto hawa ambao wanalelewa kwenye vituo, wawakumbuke kwa zawadi mbalimbali ili nao wafurahi kama watoto wengine waliopo majumbani,” amesema Shaka.
Kaimu Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Morogoro, Amisa Kagambo amesema jumla ya vituo vinne vya makao ya watoto wenye mahitaji maalumu na kituo kimoja cha kurekebisha tabia (Gereza la Wafungwa Kilosa) vimetembelewa huku akiweka bayana kuwa zaidi ya watoto 300 wameguswa na mkono wa Idd na kutumia fursa hiyo kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kusimamia zoezi hilo hadi kufanikiwa.
Sheikh wa Wilaya ya Kilosa, Nasoro Mirambo amemshukuru Rais Samia kwa kuwakumbuka watoto hao wenye uhitaji, akisema kuwa kitendo hicho ni faraja kubwa kwao, kwa wazazi wao, ndugu na hata kwa jamii nzima.