
New York. Mahakama jijini New York imeanza kusikiliza shauri linalomkabili msanii nchini Marekani, Sean Combs, maarufu P. Diddy lenye mashitaka matano ikiwemo la utumikishaji wa wanawake kingono.
Shahidi wa pili katika kesi hiyo aliyefika mahakamani jana Jumatatu Mei 12, 2025, na alitoa ushahidi wake dhidi ya msanii huyo. Shahidi huyo ni mwanaume anayefanya kazi ya kuburudisha kwenye klabu (striper) jijini New York.
Shahidi huyo, Daniel Phillip, aliieleza mahakama kuwa katika hoteli moja jijini New York, P. Diddy alimrushia mpenzi wake wa zamani, Casandra Ventura, chupa ya pombe kisha akamvuta nywele huku akimkaripia kwa lugha kali.
Philip alisema baada ya kumburuta mwanamke huyo kwa kumvuta nywele, alienda naye hadi kwenye moja ya chumba kilichopo kwenye klabu hiyo, ndipo alipoanza kusikia akimshambulia kwa kumpiga makofi.
Mbali na hilo, shahidi huyo ameileza mahakama kuwa amewahi kutakiwa, afanye mapenzi (ngono), Casandra hadharani kwa ahadi ya kulipwa fedha kati ya kipindi cha mwaka 2012 na 2013 huku Diddy akishuhudia kwa macho yake.
Phillip aliieleza mahakama kuwa kitendo hicho kilionekana kumsononesha moyo mpenzi huyo wa Diddy na hilo lilionekana wazi baada ya kutoka kwenye chumba alichokuwamo na mwanamuziki huyo.
“Aliruka ghafla kwenye mapaja yangu na alikuwa anatetemeka, mwili wake wote ulikuwa unatetemeka. Alikuwa amepigwa na butwaa,” alieleza Philip mbele ya jopo la majaji 12 na wengine sita wa akiba katika kesi hiyo maarufu inayosikilizwa kwenye mahakama ya shirikisho mjini Manhattan.
Diddy (55) amekana mashitaka yote matano ya jinai yanayomkabili likiwemo la kula njama ya kihalifu (racketeering conspiracy), biashara ya ngono, na usafirishaji wa wanawake kwa lengo la kuwatumikisha kingono.
Akikutwa na hatia kwenye makosa yote, Diddy anaweza kukumbana na kifungo kisichopungua miaka 15 jela ama kifungo cha maisha jela.
Waendesha mashitaka wanasema Combs alikuwa amewakamata kimabavu wanawake watatu, akawalazimisha kushiriki katika sherehe za ngono zilizochochewa na dawa za kulevya kwa siku kadhaa, kisha kuwarekodi video ambazo baadaye alizitumia kuwatishia nazo.
Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Elimu Johnson, aliieleza mahakama hiyo kuwa Diddy aliwaumiza wanawake kwa ukatili hususan walipokataa kushiriki katika sherehe hizo, zinazojulikana kama “Freak Offs”.
“Walipomkasirisha kwa njia yoyote ile, alikuwa akiwalazimisha kufanya hivyo,” alisema Johnson wakati wa ufunguzi wa ushahidi huo.
Kabla Phillip hajaanza kutoa ushahidi wake, majaji wanaosikiliza shauri hilo walioneshwa video ya mwaka 2016 ambapo Diddy anaonekana akimpiga Ventura, akamwangusha sakafuni katika ukumbi wa hoteli moja eneo la Los Angeles, kisha kumkanyaga alipokuwa akijaribu kuingia kwenye lifti.
Diddy, akiwa amevaa taulo tu, anaonekana akichukua vitu vya Ventura na kumburuta hadi kwenye korido.
Baadaye anaonekana akimwacha Ventura akiwa amelala sakafuni bila kujitikisa, muda mfupi kabla ya kuinuka na kuelekea kwenye eneo la ukutani ilipo simu ya hoteli.
Diddy aliomba radhi baada ya video hiyo kuonyeshwa kwa mara ya kwanza na CNN mwaka jana.
Shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka, Israel Florez, ambaye alikuwa Ofisa usalama, alieleza kuwa alipokea simu ya dharura wakati wa tukio hilo mwaka 2016.
“Aliogopa,” Florez alijibu alipoulizwa na mwendesha mashitaka kuhusu hali ya Ventura.
Florez alisema Diddy alijaribu kumpa rundo la pesa, ambalo aliliona kuwa ni hongo ya kunyamazisha kuhusu tukio hilo. Kuwa mujibu wa Florez alikataa pesa hizo.
Kesi hiyo ya Diddy imevuta hisia na ufuatiliaji mkubwa wa vyombo vya habari kutokana na umaarufu wa nyota huyo wa muziki.
“Mashahidi wengine watawaeleza kuhusu baadhi ya matukio yenye maumivu makali sana katika maisha yao. Siku walizotumia kwenye vyumba vya hoteli, wakiwa wamelewa dawa za kulevya, wakiwa wamevaa mavazi ya ajabu ili kutimiza matamanio ya kingono ya mtuhumiwa,” alisema Johnson.
Kuwa upande wake, Wakili wa utetezi, Teny Geragos, alisema katika maelezo yake ya ufunguzi kuwa waendesha mashitaka wanajaribu kugeuza uhusiano wa kimapenzi wa Diddy kuwa kesi ya kihalifu ya biashara ya ngono na ushirika wa kihalifu.
“Sean Combs ni mtu mwenye tabia tata, lakini hii siyo kesi tata. Hii ni kesi kuhusu maamuzi ya hiari yaliyofanywa na watu wazima waliokuwa kwenye uhusiano wa makubaliano,” alisema Geragos.
Kiongozi wa Jopo la Mawakili wa Diddy, Marc Agnifilo, alisema tukio la hotelini la mwaka 2016 lilikuwa ni matokeo ya ugomvi wa wivu wa mapenzi.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msanii huyo Ijumaa, Agnifilo alisema kuwa Ventura ana historia ya vurugu za majumbani, akijaribu kupinga hoja ya waendesha mashitaka kuwa alikuwa mwathirika wa ukatili wa Diddy.
Ndugu wafurika mahakamani
Miongoni wa wafuatiliaji wa kesi hiyo waliofika mahakamani ni Mama yake Diddy, Janice Combs, ambaye alikaa mstari wa mbele mahakamani akiwa na watoto sita wa Diddy.
Wakati anaingia mahakamani kwa ajili ya usikilizaji wa ushahidi wa kesi hiyo jana, Diddy alionekana akiiangalia na kuichekea familia yake huku akiwatumia mabusu hewani.
Baadaye, kesi hiyo ilipoahirishwa kwa lengo la kupata mapumziko, Diddy alitoka mahakamani akionekana kufurahia maelezo yaliyotolewa huku akirusha mikono hewani ishara ya kufurahia na kuwachekea watoto wake, mmoja wao akimrudishia ishara ya ‘ua’ akimaanisha kuwa anampenda.
Nje ya mahakama, umati wa wafuasi wa Diddy na watu wenye hamu walijazana wakirekodi video kwa simu zao za mkononi, huku wakigombea nafasi na waandishi wa habari kuiona familia ya Diddy.
Diddy anajulikana kwa kuwainua wasanii wa muziki wa Rap na R&B kama Notorious B.I.G. na Mary J. Blige hadi kuwa nyota, na hivyo kuongeza mvuto wa muziki wa Hip-Hop katika utamaduni wa Marekani miaka ya 1990 na mwanzoni mwa mwaka 2000.
Diddy pia alikuwa akikabiliwa na mashitaka zaidi ya 50 ya madai ya kisheria ya unyanyasaji wa kingono, ikiwemo moja kutoka kwa Ventura ambalo lilimalizwa kwa makubaliano ya siri.
“Jiulize kwa nini wanatoa tuhuma hizi sasa? Nia yao ni ipi? Kwa wengi wao jibu ni rahisi: pesa,” wakili Geragos alisema wakati wa ufunguzi wa ushahidi huo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.