Shahidi aeleza alivyomsaka mtuhumiwa kwenye mikoa mitatu tofauti

Dar es Salaam. Shahidi wa kwanza katika kesi ya mauaji inayomkabili mshtakiwa Isaya Mzava (63) anayedaiwa kumuua mkewe na kisha kujaribu kujiua, ameeleza namna mshtakiwa alivyokimbia nyumba yake na kwenda kujificha Muleba mkoani Kagera.

Shahidi huyo H 6760 Koplo Swalehe kutoka Kituo cha Mbweni, ametoa maelezo hayo  Mahakama Kuu Kanda ya Dar, wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo ya mauaji.

Koplo Swalehe ametoa ushahidi wake Februari 28, 2025, mbele Jaji Elizabeth Mkwizu.

Mzava anadaiwa kumuua mkewe Irene Mzava kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali, tukio analodaiwa kulitenda Desemba 28, 2021 nyumbani kwake Bunju Beach, ambapo baada ya kutekeleza mauaji hayo alitoka nyumbani kwa kutumia gari yake aina ya Harrier kwenda Kilimanjaro kisha alikimbilia Kagera alikokamatwa baadaye.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na jopo la mawakili watatu wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Yasinta Peter akishirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Ashura Mzava na Eric Kamala, shahidi huyo alidai yeye ni mmoja wa askari walioshiriki katika upelelezi wa kesi hiyo.

“Mimi ni mmoja kati askari walivyoshiriki katika upelelezi wa kesi ya mauaji nikiwa na timu ya askari wenzangu,” amedai Swalehe.

Koplo Swalehe, amedai Desemba 30, 2021, akiwa Kituo cha Polisi Mbweni, alipokea maelekezo kumfuatilia mshitakiwa Isaya Mzava.

“Tulipewa jukumu mimi na Koplo Rosta ambapo tulianza kuchukua taarifa ya  kufahamu mshtakiwa anapatikana wapi baada ya kuambiwa na msiri wetu,” amedai.

Amedai Desemba 31, 2021 saa tisa alfajiri walifika Moshi mkoani Kilimanjaro, baada ya kupata taarifa kwamba mshtakiwa yupo huko.

“Baada ya kufika Moshi tulikwenda Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Kilimanjaro na kukuta gari aina ya

Harrier limeshakamatwa ambalo alikuwa nalo mshtakiwa kabla ya kulitelekeza, hivyo nilipata taarifa kuwa yuko Kahama mkoani Shinyanga.

Tulianza safari kwenda Kahama tukaripoti kituo cha polisi Kahama tuliambiwa amekwenda mkoani Kagera Wilaya ya Muleba,” amedai.

Shahidi Koplo Swalehe, amedai waliendelea kumfuatilia mshtakiwa hadi mkoani Kagera ambapo walikuta tayari ameshakamatwa na yuko mahabusu Kituo cha Polisi Muleba.

“Mshtakiwa alikutwa na vidonda mdomoni na kwa taarifa tuliyopewa alitaka kujiua, hivyo baada ya kukamatwa sisi tulitoa taarifa kwa kiongozi wetu aliyekuwa Kituo cha Polisi Mbweni,” amesema.

Pia amedai baada ya kukamilisha kazi yao walianza safari ya kurudi Dar ambapo yeye alikwenda mkoani Kilimanjaro kuchukua gari, huku askari mwenzake  akisafiri na mshtakiwa kurudi Dar es Salaam kwa kutumia usafiri wa ndege kwani afya ya mshtakiwa haikuwa mzuri.

Mshtakiwa alivyokamatwa alifanyiwa upekuzi ambapo alikutwa na ufunguo wa gari hilo ukiwa mfukoni kwake, hivyo walipigiwa simu ndugu wa marehemu kuhusu kupatikana kwa mshtakiwa.

“Nilifanya uchunguzi ndani ya gari nikiwa na ndugu wa marehemu, hivyo  katika kiti cha nyumba kulikuwa na nguo tofauti ambazo ni fulana, vesti nyeupe yenye madoa ya damu, viatu vya  marehemu, kisu ambacho kilikuwa na damu na suruali vitu vyote vilitambuliwa na mtoto wa marehemu,” amedai.

Baada ya ushahidi huo aliomba Mahakama kupokea vielelezo ambavyo vilikuwa nje ya mahakama kisha mahakama iliamia nje kwa utambuzi wa vielelezo na vilipokelewa.

Hata hivyo, Mahakama imepokea gari aina ya Harrier rangi nyeupe kama kielelezo katika kesi hiyo pamoja na vitu vyote vilivyokuwepo ndani ya gari.

Baada ya shahidi kumaliza kutoa ushahidi, jaji Elizabeth, aliahirisha kesi hiyo hadi  Machi 3, 2025 itakapoendelea na usikilizwaji wa ushahidi upande wa mashitaka.

Mshtakiwa amerudishwa rumande, kwa sababu shitaka la mauaji halina dhamana kwa mujibu wa sheria.