Shahidi adai mama alikwenda kwa sangoma kumpumbaza bintiye

Dar es Salaam. Shahidi wa tano wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya mwanafamilia, inayomkabili Sophia Mwenda (64) na mwanaye wa kiume, Alphonce Magombola (39), ameieleza mahakama jinsi mama huyo alivyokwenda kwa mganga wa jadi na kupewa dawa ya kumpumbaza binti yake asiende Mbeya kutoa ushahidi mahakamani.

Katika maelezo ya onyo aliyotoa Kituo cha Polisi Oysterbay, Alphonce alidai mama yake baada ya kuona dawa hiyo haijafanya kazi kama alivyokusudia, alimpigia simu na kumweleza hali halisi, akimtaka aende Kijichi washauriane namna ya kumzoofisha Beatrice, ili asiende Mbeya kutoa ushahidi kwenye kesi ya kuuza nyumba ya familia kinyemela.

Mwenda, mkazi wa Mbagala anadaiwa kushirikiana na mtoto wake wa kiume, kumuua Beatrice Magombola, ambaye ni binti yake wa kwanza wa kumzaa.

Washtakiwa wanadaiwa kumuua Beatrice na kuutupa mwili wake eneo la Zinga, Bagamoyo mkoani Pwani, tukio wanalodaiwa kutenda Desemba 1, 2020, eneo la Kijichi wilaya ya Temeke.

Mshtakiwa Sophia Mwenda( alijifunika mtandio) akiwa na mwanae Alphonce Magombola, wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi yao ya mauaji kuahirishwa, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua mwanafamilia aitwaye, Beatrice Magombola. Picha na Hadija Jumanne

Mbali na kwenda kwa sangoma, Sophia katika maelezo yake ya onyo aliyoyatoa poa, pia alikiri kumuua mtoto wake ili asiende kutoa ushahidi katika kesi hiyo iliyofunguliwa na baba yake Beatrice inayotokana na Sophia akishirikiana na Alphonce kuuza nyumba iliyopo Mbeya.

Sophia na Alphonce naada ya kuuza nyumba huyo Sh45,000 waligawana fedha hizo bila kumpa taarifa mume wake, DouglasMwagombola, ambaye alifungua kesi mahakamani.

Katika mgawo wa Sh45 milioni, Sophia alipewa Sh12 milioni naye akatoa Sh1 milioni akampatia mwanaye Rachel aliyekuwa anasoma na kiasi kilichosalia alichukua Alphonce.

Shahidi Deusdedit Bachubira, ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Polisi aliyekuwa na cheo cha Sajenti, alitoa ushahidi jana Mei 16, 2025 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Kisutu.

Bachubira ametoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, aliyepewa mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi hiyo ya mauji, Mary Mrio.

Shahidi amedai alifanya mahojiano na kuandika maelezo ya onyo ya Alphonce Machi 17, 2022, ambayo mahakamani imeyapokea kama kielelezo.

Aliongozwa kutoa ushahidi na jopo la mawakili Daisy Makakala, Cathbert Mbiling’i na Violeth Davis.

Shahidi amedai alielezwa na mshtakiwa Alphonce kuwa wazazi wake walikuwa wametengana.

“Mama yangu (Sophia) walitengana na baba (Douglas Magombola) mwaka 1998 na kila mtu aliishi peke yake. Mama alikuwa anaishi Mbeya na baba alikuwa anafanya kazi Arusha,” amedai shahidi akisoma maelezo ya mshtakiwa.

“Mwaka 2008, mama yangu alianza kufanya biashara ya mazao, alichukua mkopo wa Sh15 milioni katika Benki ya NMB kwa ajili ya kilimo,” amedai shahidi.

Kupitia maelezo ya mshtakiwa amedai mama yake alishindwa kulipa mkopo huo, hivyo alimshauri wauze nyumba iliyopo mkoani Mbeya bila baba yake kujua.

Anadai Julai 2020 waliuza nyumba hiyo kwa Sh45 milioni naye akapewa Sh3 milioni, fedha nyingine mama yake alikwenda kulipa mkopo benki.

Alidai fedha nyingine alipewa Rachel ambaye ni mdogo wake.

Sahidi amedai baada ya nyumba kuuzwa familia ilianza kuhitilafiana, ndipo baba yao alipofungua kesi mahakamani.

“Novemba 2022, mama alipata taarifa kwa siri kutoka kwa mama mmoja aliyekuwa anaishi Mgeni Kaja, kuwa Beatrice anatakiwa kwenda kutoa ushahidi wa siri kwenye kesi ya baba yake mkoani Mbeya,” amedai shahidi.

Safari kwa mganga

Kupitia maelezo hayo, amedai Desemba Mosi, 2022 mshtakiwa alipigiwa simu na mama yake akimtaka aende Kijichi kwa Beatrice kwa sababu kuna ugomvi.

Alidai akiwa hapo, Beatrice alimtaka mama yake aondoke kwenye nyumba yake alikokuwa akiishi.

Kwa maelezo ya Alphonce, shahidi amedai mama yake alikwenda kwa mganga wa jadi akapewa dawa ili Beatrice ashindwe kwenda Mbeya kutoa ushahidi.

Amedai baadaye mama huyo alimweleza dawa hazifanyi kazi, hivyo aende kwa Beatrice akamuombe asimfukuze mama yao.

“Nilimwambia mama sikujui Kijichi, aliniambia atanielekeza, hivyo niliondoka Bunju, nilipofika kwa Beatrice saa 2:40 usiku nilimkuta amekaa kwenye ngazi zilizopo ndani ya nyumba yake, aliniuliza sababu ya mimi kwenda usiku bila taarifa,” amedai shahidi akinukuu maelezo ya mshtakiwa.

Baada ya muda amedai uliibuka ugomvi, Alphonce akamshika dada yake mikono na kuirudisha nyuma, kisha mama yake akamchoma kisu chini ya titi.

Amedai Beatrice aliishiwa nguvu akaanguka huku akitokwa damu, hivyo walimvingirisha shuka wakampakia kwenye gari la Beatrice aina ya Toyota Varguard na kwenda kuutupa mwili wake eneo la Zinga wilayani Bagamoyo.

“Tukiwa njiani, mama alitupa kisu alichotumia kumchoma dada kwenye bonde karibu na reli eneo la Mtoni kwa Aziz Ali. Tulifika eneo la Bagamoyo saa sita usiku na kuutupa mwili, pia tulitupa viatu, mikoba na kidongo kidogo vilivyokuwa ndani ya gari ya Beatrice. Nilimrudisha mama Kijichi,” inaelezwa katika maelezo ya mshtakiwa.

Alidai baada ya hapo alililala ndani ya gari kwenye uwanja wa CCM uliopo Kijichi, asubuhi Desemba 2, 2022 alikwenda kumchukua mtoto wa Beatrice na kwenda naye dukani kwake Makumbusho, kisha mchana walikwenda wote nyumbani kwake Bunju.

Shahidi akisoma maelezo ya mshtakiwa, amedai alipofika nyumbani kwake, mkewe alimhoji alipokuwa jana yake akamjibu alikwenda Kibaha kumchukua mtoto wa dada yake kwa kuwa Beatrice ameugua ghafla na kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu.

“Kwa kuwa sikubadilisha nguo, mke wangu aliniuliza mbona nguo zako zina matone ya damu? Nilimweleza nilikwenda gereji kupeleka gari na wakati fundi anatengeneza, nililala chini ya gari nikakatwa na bati,” amedai shahidi akisoma maelezo hayo.

Amedai ndani ya gari la Beatrice kulikuwa na mikataba ya uuzaji wa kiwanja Morogoro, vitambulisho na simu ya mkononi.

Machi 17, 2022 usiku, polisi walifika nyumbani kwake na kumkamata yeye na mke wake wakapelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay kwa mahojiano.

Baada ya ushahidi huo, upande wa mashtaka uliwasilisha ombi shahidi huyo awekwe akiba kwa muda kupisha mashahidi wengine kutoa ushahidi, kisha atatumika kwenye ushahidi mwingine.

Wakili Mbiling’i akiwasilisha ombi hilo, alieleza shahidi huyo pia alikuwa mpelelezi kwenye kesi hiyo.

Mawakili wa utetezi, Godwin Fissoo, Denis Maresa na Hilda Mushi, walipinga ombi hilo wakidai upande wa mashtaka wanataka kumtengenezea ushahidi.

Hakimu Mrio baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, alikubali ombi hilo akieleza upande wa utetezi walipewa maelezo ya mashahidi na vielelezo vyote vya kesi hiyo, hivyo upande wa mashtaka hauwezi kumtengenezea ushahidi shahidi kwa kuwa kila kitu kipo wazi na wanaweza kumhoji iwapo atatoa ambao haupo kwenye nyaraka zilizowasilishwa mahakamani.

Hakimu Mrio aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu Mei 19, 2025 saa sita mchana. Washtakiwa wamerudishwa rumande.

Uamuzi kesi ndogo

Awali, ulitolewa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya shauri la msingi uliotokana na upande wa utetezi kupinga maelezo ya onyo ya Alphonce yasipokewe na mahakama, ikidaiwa yalichukuliwa nje ya muda, pia mshtakiwa aliteswa wakati akitoa maelezo polisi.

Mahakama ilitupilia mbali pingamizi na kupokea maelezo hayo ambayo shahidi aliyasoma mahakamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *