
Shabiki wa Yanga ambaye amejitambulisha kwa jina la Malik amesema kwamba amesafiri kutoka Shinyanga kwa ajili ya kuwashuhudia watani zao, Simba wakicheza mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Stellenbosch mjini Zanzibar.
Malik ambaye alikuwa ameambatana na rafiki yake, amesema: “Nimemfuata Mnyama kwa sababu ni timu ya Tanzania. Mtani wangu ashinde fresh, hata kama tutarushiana maneno kesho mitandaoni. Ila leo ni Taifa kwanza.”
Malik alikuwa amevaa jezi ya Yanga, lakini ameonekana akiambatana na mashabiki wa Simba visiwani Zanzibar ikiwa ni siku moja kabla ya mchezo huo ambao unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa New Amaan.
Kwa miaka mingi, utani wa jadi kati ya Yanga na Simba umekuwa sehemu ya utambulisho wa soka la Tanzania. Mashabiki wa timu hizi mbili mara nyingi hujihusisha na malumbano ya maneno mitandaoni na hata kwenye maeneo ya kazi, shuleni na mitaani.
Licha ya utani huo wa muda mrefu, kuna mashabiki wachache kama Malik wanaoanza kubadili taswira hiyo kwa kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya hisia za kiushabiki.
Mchezo kati ya Simba na Stellenbosch una mvuto wa kipekee kwa sababu ni mara ya kwanza kwa Zanzibar kuandaa mechi ya hatua hiyo kubwa ya Kombe la Shirikisho, na kuifanya kuwa historia kwa visiwa hivyo.
Malik amesema alipoona tangazo la mchezo kuchezwa Zanzibar, alijua ni nafasi adimu na akaanza mipango ya safari mara moja, licha ya kuwa yeye si shabiki wa Simba.
“Nilijua huu ni wakati wa kuwa sehemu ya historia. Hii mechi ni zaidi ya Simba. Inahusu Tanzania, inahusu Afrika Mashariki. Sikuwaza mara mbili,” amesema.