
Madini ya shaba yanazidi kuibuka kwa kasi kuwa fursa kubwa katika sekta ya madini Tanzania, huku kupanda kwa bei na mahitaji duniani kukiyaweka madini haya kama rasilimali ya kimkakati yenye uwezo wa kushindana na dhahabu katika kuchochea mabadiliko ya kiuchumi nchini.
Pamoja na ukuaji wake mzuri katika soko la dunia, wataalamu wanasema Tanzania kihistoria imeweka mkazo zaidi kwenye dhahabu kutokana na bei yake ya juu katika soko la dunia.
Hata hivyo, kutokana na nafasi muhimu ya shaba katika utengenezaji wa vifaa vya umeme na nishati mbadala, saa za mkononi, wadau wanashauri Serikali iangalie upya vipaumbele vyake kwenye sekta ya madini.
Wataalamu wa madini na usafirishaji sasa wanahimiza kuwekeza kwenye mnyororo mzima wa thamani wa shaba pamoja na kuweka mazingira rafiki ya kuvutia wawekezaji zaidi.
Kwa mujibu wa Tume ya Madini Tanzania, tayari Serikali imechukua hatua kadhaa ili kuongeza uzalishaji kulingana na mahitaji ya dunia.
Hatua hizo ni pamoja na mageuzi ya kuwawezesha na kuhalalisha wachimbaji wadogo na wa kati ambao bado wanakumbwa na changamoto nyingi za kiutendaji.
Katika ziara ya hivi karibuni ya kukagua ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani ya shaba kilichopo Kata ya Mbugani, Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema kuwa ingawa kiwango cha usafishaji wa shaba inayochimbwa hapa nchini kwa sasa ni kati ya asilimia 0.5 hadi 2 pekee, kiwanda kipya kinachomilikiwa na kampuni ya Mineral Access System Tanzania (MAST) kitaweza kuchakata shaba hadi kufikia zaidi ya asilimia 70 ya usafi, akisema ni hatua kubwa katika maendeleo ya sekta hiyo.
“Ni kwa maslahi ya taifa kuhakikisha shughuli za kuongeza thamani zinafanyika ndani ya Tanzania. Hii itatuwezesha kunufaika zaidi kiuchumi kutokana na rasilimali zetu,” alisema Mavunde.
Aliipongeza MAST kwa mfumo wake wa uendeshaji unaojumuisha kuwasaidia wachimbaji wadogo kupitia mafunzo, mikopo na kununua shaba yenye kiwango cha chini cha usafi, hatua aliyoiita ya kupongezwa.
Kampuni kubwa za uchimbaji huenda zimeshatambua mabadiliko haya, na huenda ndiyo maana Barrick Gold Corporation inapendekeza kubadili jina kuwa Barrick Mining Corporation, ikiondoa neno “gold” kama ishara ya kuachana na historia yake ya kutegemea dhahabu pekee.
Barrick inawekeza dola bilioni 6 kujenga mgodi mkubwa wa shaba nchini Pakistan, ambao unatarajiwa kuanza kazi mwaka 2028 na unaweza kuendeshwa kwa zaidi ya miaka arobaini. Pia wanapanua mgodi wa shaba nchini Zambia ambao unaweza kuwa miongoni mwa migodi mikubwa zaidi duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Barrick, Mark Bristow, amekuwa akizungumzia kwa miaka mingi kuhusu kupanua uwekezaji kwenye shaba na hata alifikiria kununua kampuni za Freeport-McMoRan Inc. na First Quantum Minerals Ltd., ingawa mipango hiyo haikutimia.
Takwimu kutoka katika hifadhi data ya bei za bidhaa ya Benki ya Dunia zinaonesha kuwa bei ya shaba imepanda kwa asilimia 88 ndani ya miaka mitano, kutoka dola 5,182.63 kwa tani moja Machi 2020 hadi dola 9,739.68 Machi 2025.
Mwelekeo huu wa bei umebadilisha taswira ya soko la madini duniani, na wataalamu wanatahadharisha kuwa Tanzania inapaswa kuchukua hatua haraka kunufaika na fursa hii.
Takwimu za Tume ya Madini Tanzania zinaonesha kuwa uzalishaji wa kitaifa wa shaba umeongezeka zaidi ya mara mbili kati ya 2020 na 2025 kutoka tani 21,154.64 hadi tani 44,690.56.
Katika kipindi hicho, mauzo ya nje yameongezeka kutoka tani 13,405.03 zenye thamani ya Sh252.5 bilioni hadi tani 27,528.46 zenye thamani ya Sh533.9 bilioni.
Akizungumza na The Citizen, Annasia Kwayu kutoka Idara ya Ukaguzi wa Fedha, Mapitio ya Kodi na Ushirikishwaji wa Watanzania wa Tume ya Madini alisema kuwa sekta hiyo inashuhudia ukuaji katika maeneo ya utafiti, uchakataji na uchimbaji, hasa kwa wachimbaji wa kati na wadogo.
Alibainisha kuwa uzalishaji wa shaba unaweza kufikia tani 205,713.88 ifikapo mwaka 2030, iwapo kiwango cha ukuaji wa wastani wa kila mwaka wa asilimia 15.08 kitaendelea.
Mtaalamu wa madini kutoka ASNL Advisory Limited, Humphrey Simba anasema wakati umefika kwa shaba kupewa uzito unaostahili.
“Ni wakati wa Serikali kuweka kipaumbele kwenye shaba. Shaba ni muhimu sana katika utengenezaji wa nyaya za umeme na inahitajika sana na viwanda vya vifaa vya umeme duniani. Shaba sasa ndiyo kigeuza mchezo,” alisema.
Akiunga mkono hoja hiyo, Mkuu wa Biashara wa Sas Logistics Limited, Alex Lugendo alitaja ongezeko kubwa la mahitaji ya madini hayo duniani, hasa kutoka China na Korea Kusini, na akatoa wito wa mkakati wa kitaifa wa kuchangamkia fursa hiyo.
“Kuna fursa halisi kwenye uchimbaji wa shaba. Tunapaswa kushirikisha wadau, kurahisisha taratibu za kuvuka mipaka, kutatua changamoto za kisheria na kuimarisha mifumo ya usafirishaji kama tunataka kutumia fursa hii,” alisema.
Lugendo pia alitaja maboresho ya miundombinu ya bandari kuwa yanasaidia katika kuboresha mzunguko wa mizigo. “Kampuni yetu husafirisha kemikali kwenda DRC na kurejea na shehena ya shaba. Hii inaonesha upanuzi wa biashara za kikanda.”
Wakati huohuo, mjiolojia na aliyewahi kuwa Kamishna wa Madini, Dk Dalaly Kafumu alisisitiza umuhimu wa kujenga mnyororo imara wa thamani wa shaba na kukuza viwanda vya ndani.
“Tuna kiwanda cha kutengeneza nyaya ambacho kwa sasa kinaagiza shaba kutoka nje. Tukianza kuchakata hapa nchini, tutapunguza gharama na utegemezi wa uagizaji. Kufanyia mapitio sheria za madini ili kuvutia wawekezaji ni muhimu sasa hivi ambapo shaba ni madini ya kimkakati yenye mahitaji makubwa,” alisema.
Dk Kafumu pia alibainisha kuwa ingawa dhahabu mara nyingi husafirishwa ghafi, kuongeza thamani kwenye shaba kunaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya taifa.