Sh970 milioni zatengwa kusaidia wenye ulemavu

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kipindi cha miaka mitatu imetenga Sh970.810 milioni kwa ajili ya usaidizi wa kundi la watu wenye ulemavu zikijumuisha ununuzi wa vifaa saidizi kulingana na mahitaji yao.

Hatua hiyo itawawezesha kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii, kielimu na kiuchumi.

Hayo yamebainishwa leo Mei 17, 2025 katika mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman.

Amesema katika kutambua changamoto za kundi hilo, Serikali imeanzisha mfuko wa maendeleo kwa ajili ya kuwasaidia.

Waziri amesema kwa mwaka ujao wa fedha 2025/26 mfuko huo umetengewa Sh490.810 milioni, mwaka 2024/25 mfuko ulitengewa Sh280 milioni, huku mwaka 2023/24 zilitengwa Sh200 milioni.

Amesema kuna mikakati mingine ya kuendeleza ushirikiano kwa kukaribisha taasisi na wadau wenye lengo la kutoa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu.

Amesema mwaka 2023 hadi mwaka huu jumla ya vifaa saidizi 1,277 vyenye thamani ya Sh443.9 milioni vimetolewa Unguja na Pemba.

Waziri amesema Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu hufanya tathmini ya mara kwa mara kwa lengo la kubaini mahitaji ya vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu, kuratibu upatikanaji na ugawaji wa vifaa hivyo kwa ufanisi zaidi.

Waziri alikuwa akijibu swali la Mwantatu Mbaraka Khamis (nafasi za wanawake) aliyetaka kujua mikakati ya Serikali kuhakikisha watu wnye ulemavu wananufaika kwa kupatiwa vifaa hivyo na kiasi gani cha bajeti kinatengwa kwa kila mwaka kwa ajili ya kununua vifaa saidizi.

Miradi hifadhi ya jamii

Katika hatua nyingine, Sh279.260 bilioni zimewekezwa katika utekelezaji wa miradi kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1998.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Juma Makungu Juma amesema hayo leo Mei 17, 2025 barazani akijibu swali la mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman aliyetaka kujua kiwango kilichowekezwa kwenye miradi tangu mwaka 1998.

Pia alitaka kujua faida gani imepatikana kwa ZSSF na wachangiaji wakuu na hasara za uwekezaji huo katika miradi iliyofanywa na mfuko huo.

Makungu amesema uwekezaji huo umefanywa katika miradi ya majengo ya biashara, makazi, viwanja vya michezo ya watoto na miundombinu mbalimbali.

Kuhusu faida iliyopatikana tangu kuanza uwekezaji huo hadi kufikia mwaka 2023/24 amesema ni Sh88.809 bilioni.

Akizungumzia faida inayopatikana kwa wachangiaji amesema: “Miradi hiyo imezalisha ajira mbalimbali za kudumu na za muda mfupi, lakini pia imeongeza na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.”

Mfuko umelipa mafao kwa wakati kulingana na sheria na taratibu zilizowekwa, huku ukichangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ukwasi na kusababisha mfuko kuongeza mafao hadi kufikia sita kutoka matatu ya awali.

Ameyataja mafao hayo kuwa kiinua mgongo na pensheni, ulemavu, urithi, uzazi, ukosefu wa ajira na mafao ya fidia ya kuumia kazini.

Naibu waziri amesema mafao hayo hulipwa kutokana na faida ya fedha zinazotokana na miradi ya uwekezaji inayofanywa na mfuko.

Kuhusu hasara za uwekezaji katika miradi iliyofanywa za ZSSF, amesema tangu mfuko huo uanzishwe haujawahi kupata au kuripoti hasara katika uendeshaji wake, ila kumejitokeza baadhi ya changamoto za kibiashara ambazo zinasababishwa na mabadiliko ya kiuchumi duniani.

“Changamoto ambazo husababisha miradi yetu ya uwekezaji wakati mwingine kupata faida chini ya kiwango kilichowekwa ukilinganisha na matarajio ya mfuko. Hili hutokea mara chache hasa wakati wa mabadiliko ya viwango vya faida vya uwekezaji kwenye masoko ya fedha ya ndani na nje ya nchi, au vipindi vya mporomoko wa uchumi wa dunia,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *