
Unguja. Ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, umezinduliwa mradi katika sekta ya elimu wa Dola za Marekani 3.6 milioni sawa na Sh9.6 bilioni unaotarajiwa kuwafikia vijana 116,080 kisiwani Zanzibar.
Kati ya vijana hao, 110,480 ni wanafunzi kutoka shule 216 za sekondari Unguja an Pemba na 5,600 ni vijana wanaotoka katika mfumo usio rasmi wa elimu.
Akitoa taarifa za kitaalamu wakati wa kuzindua mpango huo leo Aprili 22, 2025, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Khalid Waziri amesema wanafunzi hao watapewa mafunzo ya kuandaa vitalu vya miti na kusambaza katika shule zote za Zanzibar kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.
“Zaidi ya vijana 100,000 waliopo nje watafundishwa maarifa, ujuzi na hatua madhubuti za kuchukua katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa maendeleo endelevu,” amesema Waziri.
Mpango huo unadhaminiwa na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef) kwa kushirikiana na Taasisi ya Education Above All (EAA) ya nchini Qatar kupitia Mpango wake wa Reach Out to Asia (Rota).
Katika mpango huo wa miaka miatatu, miti 300,000 ikiwemo mikoko, mikaratusi na mizambarau itapandwa na tani laki moja za chakula cha mbogamboga zitazalishwa kupitia mradi huo.
Kwa mujibu wa waziri, pia lita laki nne za maji zitavunwa na kutumika katika mradi huo kwa matumizi mbalimbali ya kilimo na tani 120,000 zitakazozalishwa shuleni zitachakatwa na kutoa tani 28,000 za mbolea, itatumika katika miti itakayopandwa.
Amesema lengo la mradi huo ni kuongeza maarifa na ujuzi kwa wanafunzi wa shule za sekondari na vijana walionje ya mfumo rasmi wa elimu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuchukua hatua madhubuti dhidi ya athari za mabadiliko hayo kwa maendeleo ya Zanzibar.
Mradi huo wa miaka miatatu utajikita katika maeneo makuu matano miongoni mwayo ni pamoja na kutekeleza elimu ya mabadiliko ya tabianchi katika ngazi zote kuanzia maandalizi hadi sekondari.
Pia, kutoa mafunzo kwa walimu ili wafundishe elimu ya mazingira kwa ufanisi, kuweka mazingira rafiki yanayoizunguka shule kwa kujifunza, kuwawezesha wanafunzi wa rika tofauti kwa ajili ya kupeleka elimu kwenye jamii waanzotoka, kuwaelewesha vijana kutambua mabadiliko ya hali ya hewa ili kupunguza athari zake.
Mwakilishi wa Unicef Tanzania, Elke Wisch amesema Zanzibar inakabiliwa na tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa kutokana na kuongezeka kwa viwango vya bahari hadi mmomonyoko wa pwani na mvua zisizo sawa hivyo kutishia jamii na maisha
“Kwa kuwapa watoto na vijana wenye ustadi wa vitendo, mpango huu unawapa vifaa vya kuongoza hatua za hali ya hewa na kuendesha mabadiliko endelevu kutoka chini na kusaidia kujenga mustakabali zaidi na endelevu kwa wote,” amesema mwakilishi huyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Programu ya Rota, Abdulla Al Abdulla amesema katika elimu juu ya msingi, “Tunaamini vijana siyo tu wanufaika wa mabadiliko ya hali ya hewa bali ni nguvu ya pamoja ya kuendesha mpango huo, vijana ni kizazi cha kulinda mazingira.
Katika hotuba yake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema Zanzibar haipo salama dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwani visiwa hivyo vimeanza kushuhudia athari hizi katika maeneo mbalimbali.
“Katika maeneo ya Pwani, mmomonyoko wa ardhi umeharibu kwa kiasi kikubwa miundombinu ya kiutalii pamoja na makazi ya wananchi na wakulima katika maeneo yao ya kilimo wanakabiliana na mabadiliko ya misimu ya mvua na ukame wa muda mrefu, hali inayosababisha kushuka kwa uzalishaji wa chakula na kuongeza gharama za maisha,” amesema Othman.
Othman amesema athari hizi siyo tu zinatishia ustawi wa wananchi bali zinahatarisha kasi ya maendeleo yakiwemo ya uchumi na hali hiyo inakumbusha mabadiliko ya tabianchi si suala la kesho bali ni changamoto ya sasa inayohitaji hatua madhubuti.
Othman amesema kwa kuzingatia hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) umeweka mkazo maalumu katika kuhakikisha vijana wanajengewa uwezo wa kuelewa kwa kina na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya athari hizo.
Ameeleza kuwa, Serikali inaamini kuwa mapambano dhidi ya tabianchi hayawezi kufanikiwa bila kuwawezesha vijana kwa kuwapa maarifa, stadi na uelewa sahihi kuhusu masuala hayo.
Kupitia mradi huu, shule zetu zitajengewa uwezo wa kufundisha na kukuza uelewa wa masuala ya tabianchi kwa wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla, sambamba na kuimarisha miundombinu ya elimu inayostahamili athari za mabadiliko hayo,” amesema.
Othman amesema, uzinduzi wa mradi huo katika Mkoa wa Kaskazini siyo jambo la bahati nasibu bali ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuimarisha hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa njia jumuishi, shirikishi na endelevu.