
Geita. Licha ya Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kutenga Sh8 bilioni kwa ajili ya mikopo ya riba nafuu kwa wafanyabiashara wadogo, hadi sasa ni Sh700 milioni pekee zilizokopwa.
Mwitikio mdogo wa kuchukua mikopo hiyo umekuwa changamoto, licha ya nia ya Serikali ya kuwawezesha wafanyabiashara wa kipato cha chini kuongeza mitaji yao na kuboresha maisha yao kiuchumi.
Fedha hizo zilitolewa tangu Machi 2025 zikiwa na lengo la kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kuongeza mitaji yao na kujikwamua kiuchumi. Hata hivyo, mwitikio wa kuzichukua umekuwa mdogo mno.
Akizungumza katika ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita leo, Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara hiyo, Carlos Gwamagobe amesema Serikali imeweka fedha hizo benki tayari kwa ajili ya kukopesha, lakini hadi sasa ni wafanyabiashara wawili pekee kutoka Geita waliojitokeza kuomba na kupewa mikopo hiyo, licha ya zaidi yawa tu 100 kupewa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo.
“Hadi sasa fedha bado zipo benki, lakini hazitumiki, na imebaki miezi miwili kabla mwaka wa fedha kuisha. Tumekuja Geita kufahamu ni changamoto gani zinazowazuia wafanyabiashara kuiomba,” amesema Gwamagobe.
Amebainisha kuwa moja ya masharti ya msingi ya kuomba mkopo huo ni kuwa na kitambulisho cha mfanyabiashara mdogo kinachotolewa kwa waliojisajili rasmi.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo Mkoa wa Geita, Maulid Said amesema pamoja na jitihada nzuri za Serikali, bado kuna changamoto katika utekelezaji wa mpango huo, hasa kwenye taasisi ya fedha inayosimamia utoaji wa mikopo.
“Wafanyabiashara wengi wamejisajili, lakini hawajapata mikopo. Zaidi ya watu 20 hapa Manispaa ya Geita wamewasilisha maombi, lakini hadi sasa hawajapokea majibu wala fedha. Tunaamini tatizo lipo kwenye taasisi ya fedha, hivyo tunaiomba Serikali iangalie upya utaratibu huu,” amesema Said.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Geita, Martha Kaloso amesisitiza umuhimu wa kila mkoa kupewa taarifa rasmi kuhusu mgawo wa fedha hizo, ili kurahisisha ufuatiliaji na usimamizi wa karibu.
Akihitimisha kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, amesema kuna haja ya kuimarisha elimu kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa usajili na fursa zinazopatikana kupitia vitambulisho, ikiwemo mikopo ya riba nafuu.
“Mikopo hii ni kwa ajili ya Watanzania wote. Tukishirikiana, tunaweza kusaidia wafanyabiashara kujikwamua kiuchumi na kuchangia katika ukuaji wa mapato ya mkoa na Taifa,” amesema Gombati.