Sh6 Bilioni kuimarisha uzalishaji na usalama wa chakula

Unguja. Ili kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa chakula kwa kuimarisha sekta za misitu, kilimo, maji, na ardhi, umetambulishwa mradi wa Dola milioni 2.35 za Marekani (Sh6.042 bilioni) kisiwani Zanzibar.

Mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Duniana Global Environmental Fund (GEF) unatarajiwa kutekelezwa kwa miaka mitano kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza wakati wa kutambulisha mradi huo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja leo Jumatatu, Machi 10, 2025, Mratibu wa Mfumo wa Chakula, Matumizi na Urejeshaji wa Ardhi Tanzania, Miza Suleiman Khamis, amesema lengo ni kukuza usimamizi jumuishi wa rasilimali ardhi na maji, pamoja na urejeshaji wa mnyororo wa thamani wa zao la mpunga ili kuzuia ukataji holela wa miti unaoharibu ardhi.

“Mradi huu pia unalenga kuimarisha maeneo yaliyokatwa miti kwa kutekeleza mifumo bora ya kilimo na matumizi ya maji na ardhi,” amesema Miza.

Miongoni mwa wadau wanaoshirikiana kuendeleza mradi huu ni wataalamu wa ardhi, kilimo, na maji, pamoja na watendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (Zari), Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa), Halmashauri za Mkoa wa Kaskazini Unguja, na Idara ya Mazingira.

Miza, ambaye pia ni Ofisa Mkuu katika Idara ya Misitu Zanzibar, amesema lengo lingine ni kuimarisha ushirikiano baina ya wadau mbalimbali ili kutatua changamoto zilizopo na kuyaimarisha maeneo yaliyoharibiwa kwa ajili ya kuendelea na shughuli za kilimo.

Ameeleza kuwa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar inaendelea na hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo kukamilika kwa kikao cha kwanza cha Kamati ya Uendeshaji kilichopitisha mapendekezo ya mpango wa utekelezaji, ikiwa ni pamoja na bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Hivyo, kukamilika kwa hatua hiyo kumetoa fursa ya kuanza utekelezaji wa shughuli za mradi unaotarajiwa kusaidia kurejesha maeneo yaliyoharibika kwa kushughulikia makinga maji ili kuongeza uzalishaji wa mpunga unaoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema wananchi wa maeneo ya utekelezaji wa mradi watanufaika kwa kupata uwezo wa kuendeleza uzalishaji katika mkoa huo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mattar Zahor Masoud, ameahidi kutoa ushirikiano katika kila hatua ili kuhakikisha mradi unafanikiwa na kuleta tija katika sekta ya kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *