Sh52.3 bilioni zatumika ujenzi wa Mahakama za mwanzo 60 nchini

Sh52.3 bilioni zatumika ujenzi wa Mahakama za mwanzo 60 nchini

Geita. Katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na bila usumbufu wa kutembea umbali mrefu, Mahakama ya Tanzania inatekeleza ujenzi wa mahakama za mwanzo 60 katika maeneo mbalimbali nchini zinazojengwa kwa gharama ya Sh52.3 bilioni.

Fedha hizo ni sehemu ya mkopo wa riba nafuu kutoka Benki ya Dunia kupitia mpango wa maboresho ya huduma za  utoaji haki.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel ameyasema hayo leo Mei 21, 2025 wakati akitoa taarifa ya maboresho ya miundombinu ya majengo ya Mahakama nchini, na kusema ujenzi huo unaenda sambamba  na juhudi za kusogeza huduma kwa wananchi na kuboresha mazingira ya utoaji haki.

“Mahakama hizi zinatarajiwa kukamilika ifikapo Juni mwaka huu na zitapunguza changamoto za wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta haki, tofauti na zamani sasa huduma zinapatikana karibu ndani ya kilomita tano kwa maeneo mengi nchini,”amesema Profesa Ole Gabriel.

Mbali na ujenzi wa Mahakama za Mwanzo pia Mahakama inatekeleza ujenzi wa vituo jumuishi tisa vya kisasa vinavyohusisha Mahakama za ngazi zote kuanzia ya mwanzo hadi rufani.

Mikoa inayotekeleza miradi hiyo ni Geita, Simiyu, Njombe, Katavi, Songea, Lindi, Singida Songwe na Pemba.

Profesa Ole Gabriel amesema mradi huo wa vituo jumuishi unatekelezwa kwa gharama ya dola milioni 90 za Marekani sawa na Sh203 bilioni ambazo ni fedha za mkopo awamu ya pili kutoka Benki Dunia.

“Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa iliyopata vituo hivi na kama mnavyoona jengo limepiga hatua hadi sasa utekelezaji ni asilimia 88 na tunatarajia kuja kuzindua ifikapo Juni, ambapo hapa utazinduliwa kwa niaba ya maeneo yote yenye vituo hivi,”amesema.

Aidha, Mahakama ya Tanzania inatekeleza ujenzi wa nyumba za majaji, na ukarabati wa Mahakama Kuu ya Musoma, Iringa na Dodoma ambapo amesema iliyokuwa Mahakama Kuu Dodoma, inakarabatiwa na kuwa  maalumu kwa ajili ya kushughulikia mashauri ya kifamilia.

Profesa Ole Gabriel amesema majengo yote yanayojengwa yamezingatia matumizi ya Tehama, vigezo vya upatikanaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu na mazingira rafiki ya kazi kwa watoa haki.

“Kwa ujumla, maboresho haya ni chachu ya mageuzi katika upatikanaji wa haki kwa Watanzania. Tunataka wananchi wapate haki kwa wakati, usawa na bila usumbufu wa umbali wala gharama kubwa,” amesisitiza.

Wakizungumzia maboresho katika miundombinu ya Mahakama baadhi ya wananchi wa Geita wamesema yamewasaidia wananchi wa Geita waliokuwa wakilazimika kusafiri kwenda Mwanza kutafuta haki.

Emanuel Magesa mkazi wa Bomani Manispaa ya Geita amesema mkoani humo hakukuwa na mahakama kuu, hivyo wananchi walilazimika kusafiri hadi Mwanza kusikiliza mashauri yao hasa zile kesi za mauaji na jinai.

“Hata hii Tehama imekua ya mfano sasa hivi Geita mfungwa anaweza kuwa Butimba Mwanza na Jaji yupo Geita na kesi ikaendelea bila yeye kuwepo Geita  na mnamuona, haya ni maendeleo makubwa kwenye mahakama zetu,”amesema Magesa.

Lilian Evarist mkazi wa Bombambili Mjini Geita amesema maboresho ya miundombinu ya mahakama yamewaondolea wananchi changamoto ya kutembea umbali mrefu kwa kuwa sasa wilaya zote zina mahakama, hivyo washtakiwa na mashahidi hawalazimiki kusafiri hadi Geita na badala yake kesi zinasikilizwa kwenye wilaya husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *