
Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuanzia bajeti ya mwaka mpya wa fedha 2025/2026, wizara itaanza kutenga Sh5 bilioni kila mwaka kwa ajili ya kugharamia masomo ya data science, machine learning na akili mnemba (AI).
Amesema licha ya kuwa kiwango hicho ni kidogo, lakini kinaweza kufungua milango ya fursa kwa vijana wengi nchini.
Fedha hizo zitatumika kuwasomesha vijana katika maeneo hayo ya teknolojia ya kisasa, hatua ambayo inalenga kuchochea maendeleo ya kiteknolojia na ubunifu nchini.
Profesa Mkenda aliyasema hayo jana jioni Alhamisi Aprili 17, 2025, wakati wa hafla ya utiaji saini ya makubaliano kati ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na CRDB Bank Foundation kuhusu utoaji wa mikopo nafuu kwa wabunifu wa Kitanzania.
Tayari Serikali imetenga Sh2.3 bilioni kwa ajili ya mikopo hiyo, huku CRDB ikiongeza kiasi kama hicho, hivyo kufanya jumla ya fedha zinazopatikana kufikia Sh4.6 bilioni.
Akiangazia umuhimu wa kuwekeza katika masomo ya teknolojia ya kisasa, Profesa Mkenda alisema dunia ya sasa haiwezi kuepuka masuala ya data science na AI kwa kuwa ni maeneo yenye mchango mkubwa katika utoaji wa ajira.
Alifafanua kuwa fedha zitakazotengwa kwa ufadhili hazitapitishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, bali zitapelekwa moja kwa moja Costech kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo.
Amebainisha kuwa Watanzania wengi, hususan waliotoka shule za kawaida, hawajitokezi kuomba ufadhili wa masomo nje ya nchi tofauti na wale waliosoma shule za kimataifa.
Hivyo, waziri huyo alisema ili kuhimiza ushiriki wa vijana wote, Serikali itatangaza nafasi za ufadhili huo kwa vigezo vya wazi, ikiwalenga wahitimu wa kidato cha sita na wale wanaotafuta shahada ya kwanza.
“Wale watakaofaulu watawekwa kwenye chuo maalum kwa mwaka mmoja kwa ajili ya mafunzo ya awali ya kidijitali, ikiwemo kuwapa uzoefu wa kimataifa, huku Costech ikisimamia maandalizi hayo na Serikali ikitafuta udhamini wa masomo au kuwalipia moja kwa moja,” alisema Profesa Mkenda.
Kuhusu mikopo ya biashara bunifu, Profesa Mkenda alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dirisha maalum la mikopo lililozinduliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko.
“Dirisha hilo linatoa fursa kwa vijana wabunifu walioko hatua ya kuingiza bidhaa sokoni kupata mitaji, huku Serikali ikitoa dhamana kupitia mfumo unaoratibiwa na Costech na CRDB Bank Foundation,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu alisema mchakato wa maombi ya mikopo hiyo utaendeshwa kwa uwazi na waombaji watapaswa kuwasilisha taarifa za mradi pamoja na mpango wa biashara.
Amesisitiza kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi ili kuondoa dhana kwamba vijana hawawezi kukopeshwa kwa sababu hawana dhamana, kwa kuwa katika mpango huu, Serikali ndiyo mdhamini.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa, amesema ili kuhakikisha uwajibikaji wa kifedha, mazingira ya upatikanaji wa mikopo hiyo yameboreshwa. Miongoni mwa vigezo vitakavyozingatiwa ni mikataba ya biashara, nyaraka za malipo, historia ya uaminifu, uwezo wa kukuza biashara, na uwezo wa kurejesha mkopo.
Amesema makubaliano hayo yatachochea ukuaji wa biashara changa na kuhakikisha fedha zinawafikia walengwa kwa wakati.