
Unguja. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema wataendelea kuimarisha misitu katika maeneo yaliyoharibiwa ili kuongeza uzalishaji na usalama wa chakula nchini.
Mratibu wa Mradi wa Mfumo wa Chakula, Matumizi na Urejeshaji wa Ardhi, Miza Suleiman Khamis, Amesema hayo leo Jumapili, Januari 26, 2025, wakati akiwasilisha andiko la mradi huo utakaoshughulikia maeneo yaliyokatwa miti, pamoja na kuweka mifumo bora ya maji ardhini.
Mratibu huyo amesema mradi huo utawezesha kukuza usimamizi jumuishi wa rasilimali za ardhi na maji, pamoja na urejeshaji wa mnyororo wa thamani wa zao la mpunga ili kuzuia ukataji wa miti na uharibifu wa ardhi.
“Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar inaendelea na hatua za awali za utekelezaji wa mradi huu, ikiwemo kukamilika kwa kikao cha kwanza cha kamati ya uendeshaji ambacho kilipokea na kupitisha mapendekezo ya mpango wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025,” amesema Miza.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa hatua hiyo kumetoa fursa ya kuanza kwa utekelezaji wa shughuli za mradi huo, unaotarajiwa kusaidia maeneo yaliyoharibika, yakiwemo ya hifadhi za misitu na maeneo ya kilimo cha mpunga.
Pia, amesisitiza kuwa mradi huo utashughulikia makinga maji yatakayosaidia kuimarisha uzalishaji zaidi wa mpunga kutokana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Awali, mmoja wa waandaji wa mradi huo, Saleh Kombo Khiar, amesema mradi huo umebeba dhana mpya ambayo itaweza kuangalia mandhari nzima ya eneo na utajumuisha sekta mbalimbali nchini.
Hivyo, amewataka wananchi watarajie mafanikio makubwa katika mradi huo kwa kuwa utaenda kuboresha maeneo yaliyoharibika na kuwa na mtazamo wa maendeleo kisiwani hapa.
Kwa upande wake, Ofisa Uzalishaji kutoka Idara ya Umwagiliaji, Rukia Wahabi Mohamed, amesema mradi huo utakuwa na fursa nyingi kwa wananchi kutokana na malengo yake ya kukuza matumizi bora ya ardhi na mnyororo wa thamani wa zao la mpunga.
Mradi huo wa kuendeleza mifumo ya chakula, matumizi na urejeshaji wa ardhi unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kupitia Idara ya Misitu.
Mradi huo utatekelezwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) na Global Trust Fund, ambapo Dola milioni 2.3 za Marekani, sawa na Sh5.98 bilioni, zitatumika katika mradi huo kwa kipindi cha miaka mitano.