Sh5.5 bilioni kuyaongezea ujuzi makundi ya vijana sekta hizi

Unguja. Vijana 711,880 kutoka makundi tofauti wanatarajiwa kuongezewa ujuzi kulingana na fani zao nchini kupitia mradi wa vijana Plus.

Mradi huo unaoanza mwaka huu hadi 2026, utawapa fursa vijana katika sekta tofauti wakiwemo wajasiriamali, wasanii na waandishi wa habari ili kuwaongezea ujuzi katika maeneo wanayofanyia kazi kwa kipindi cha miaka mitatu utagharimu Euro 2.2 milioni (Sh5.5 bilioni).

Akizungumza katika hafla fupi ya utambulisho wa mradi huo leo Alhamisi Machi 6, 2025, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaib Ibrahim Mohamed amesema utasaidia kuwajengea uwezo vijana katika usimamizi na utekelezaji wa mashirika yao ili kuepukana na changamoto zinazowakwamisha.

“Hata hivyo ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa ipasavyo na kuleta tija lazima kuwapo na ushirikiano wa karibu na wadau, kwani utasaidia kuimarisha ustawi na maendeleo ya vijana,” amesema.

Amesema licha ya wizara hiyo kusimamia na kuratibu maendeleo ya vijana, utekelezaji wa maendeleo hayo hutekelezwa na wadau mbalimbali wa sekta binafsi, kutoka ndani na nje ya nchi na Serikali.

Naye mtaalamu wa Ulinzi na Utawala wa Haki za Watoto kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani, (Save the Children), Barnabas Kaniki amesema lengo la mradi huo ni kuyawezesha mashirika ya vijana na viongozi wake kuwa wadau wakuu kwenye masuala ya utawala bora na maendeleo.

Amesema vijana watakaolengwa kupatiwa fursa hiyo katika mradi huo ni kati ya umri wa miaka 15 hadi 29 katika kanda tano zikiwamo Dodoma, Mwanza, Tanga, Zanzibar, Mtwara, Mbeya, Kigoma na  Morogoro.

“Mradi huu utawajengea uwezo vijana wa mashirika 40 kwa kuzitatua changamoto zilizopo na kuwapa elimu viongozi wao 100 kutoka katika mashirika hayo ili kuwajengea uwezo kiufanisi,” amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi kutoka Tanzania Bora Initiative, Alfred Kiwuyo amesema matarajio ni kuwafikia vijana wengi ambao hawajafikiwa ili kuwafungulia njia za maendeleo.

Katika utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la kuhudumia watoto la Save The Children na Tanzania Bora Initiative, yatafanyika makongamano mbalimbali ili kuwapa fursa vijana wa sekta hizo.