Sh400 bilioni kutumika miradi ya maendeleo Mbeya

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera amesema  Serikali imepitisha bajeti zaidi ya Sh400 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa lengo la kusogeza huduma muhimu kwa wananchi.

Miongoni mwa miradi itakayotekelezwa ni pamoja na jengo la utawala la Ofisi ya Mkurugenzi wa  Halmashauri ya Jiji la Mbeya,  ambalo  tayari Wizara ya Tamisemi imetoa maelekezo  kujengwa   katika eneo la Uyole   Kata ya Uyole jijini hapa.

Dk, Homera ametoa kauli hiyo usiku wa Jumatano Machi 27, 2025 wakati akitoa salama za Mkoa kwa wananchi, waumini wa  Kiislamu, viongozi wa chama na serikali kwenye  futari iliyo andaliwa na Spika wa Bunge na Mbunge Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson.

Homera amesema hivi karibuni  wakuu wa mikoa walikuwa jijini Dodoma kwa ajili ya kupitisha  bajeti za kutekeleza miradi ya maendeleo, huku kwa Mkoa wa Mbeya ikipitishwa bajeti kubwa ya zaidi ya Sh400 bilioni.

“Tunaona namna gani serikali ya awamu ya sita inavyotenga bajeti kwa ajili ya kusogeza huduma muhimu kwa wananchi lakini pia nimshukuru Mbunge wa Mbeya mjini na Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson namna ambavyo pambana kuona miradi ya kimkakati inawafikia  wananchi,” amesema

Dk Homera amesema mbali na serikali kuleta fedha hizo kwa ajili ya miradi ya maendeleo hususani ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Jiji lakini  Mbeya imepiga hatua katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

“Tunaona kuna mradi wa barabara njia nne unaendelea sambamba na ule wa maji wa chanzo cha mto Kiwira ambao utakuwa suluhisho la maji kwa baadhi ya maeneo katika Mkoa wa Mbeya na mikoa ya jirani,” amesema.

Wakati huohuo, Dk Homera amewataka wananchi  kufanya dua na maombi kuombea   uchaguzi Mkuu ambao unaotarajiwa kufanyika  Oktoba, 2025  hususani kwa nafasi ya Rais Samia Suluhu Hassan  na wabunge akiwepo Dk Tulia Ackson.

“Tunapaswa kumuunga mkono, Dk Tulia sio kwa maneno bali kwa kitendo, sasa tunaelekea kwenye uchaguzi kwa upande wa nafasi ya  Rais Samia Suluhu tayari kuna mgombea mwenza ambaye ni Dk Emmanuel Nchimbi,” amesema.

Akizungumza na maelfu ya wananchi walioshiriki kupata futari, Spika Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson,  kwanza ameanza kwa kushukuru huku akisisitiza kufanya dua la kuliombea taifa katika kuelekea kipindi cha uchaguzi Mkuu pasipo kujali itikadi za vyama.

Kuhusu serikali kutoa fedha kwa ajili ya  ujenzi wa miradi ya maendeleo hususani jengo la kisasa la  utawala amesema lengo ni kuonyesha taswira ya Jiji la Mbeya ili kusogeza huduma muhimu kwa Watanzania.

Amesema viongozi  wa chama (cha mapinduzi) na serikali wana wajibu wa kusimama na kueleza wananchi nini  serikali imefanya nini katika kuleta maendeleo ya kwa kipindi cha miaka minne.

“Ibada ya futari  huwa  inafanywa kila mwaka, lakini  ya mwaka huu hii iwe ya tofauti kwa sababu tunaelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 ,niwaombe  waumini  tumuombee  Rais Samia Suluhu Hassan awe na afya njema, huku sisi wengine tuombeeni maombi ya jumla,” amesema.

Amesisitiza maombi kwa nafasi ya Urais ni lazima ,lakini kwa upande wake, Dk Tulia hana  mashaka kwa sababu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo yaliyoletwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaonekana.

Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Ayas Njalambaha amewakumbusha na kuwasisitiza  waumini wa dini ya Kiislamu kuliombea taifa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu .

“Ndugu zangu huu ni wakati wa kuelekeza macho yetu kufanya dua la kuombea taifa na viongozi wetu wakuu wa nchi, lakini pia kwa hii tunu ya Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson kutoipoteza,” amesema.

Njalambaha, amesema kimsingi kama viongozi wa dini wanatambua mchango mkubwa unaofanywa na kiongozi huyo wa kidunia na hawako tayari kumpoteza.

Mmoja wa washiriki katika hafla ya kupata futari, Hawa Juma amesema kila Mtanzania kwa imani yake ni kipindi cha kushikamana kufanya dua kukemea mihemko ya kisiasa ambayo itaweza kuleta machafuko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *