
Arusha. Serikali imetenga jumla ya Sh4 bilioni kwa ajili ya kufanikisha kazi ya kuhesabu wanyama pori walioko nchini katika msimu wa mwaka 2025/2026.
Lengo la sensa hiyo ya kitaifa, inayoratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori Tanzania (Tawiri), ni kusaidia juhudi za uhifadhi wa wanyama pori na kuchangia katika kuimarisha sera za uhifadhi na usimamizi wa wanyama pori nchini.
Kwa mujibu wa sensa ya wanyama pori ya msimu wa mwaka 2024 iliyotolewa na Tawiri, ilibainisha kuwa Tanzania kinara wa idadi kubwa ya nyati na simba barani Afrika.
Kwa upande wa nyati, Afrika nzima wapo 401,000 ambapo Tanzania pekee wapo 225,000, ikifuatiwa na Afrika Kusini (46,000), Msumbiji (45,000), Kenya (42,000), na Zambia (41,000).
Kwa upande wa simba, Tanzania inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama hao, ambapo kati ya 29,000 waliopo barani Afrika, 17,000 wapo nchini, ikifuatiwa na Afrika Kusini (3,284), Botswana (3,064), Kenya (2,500), na Zambia (2,500).
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi wa Utafiti wa Wanyama Pori kutoka Tawiri, Julius Keyyu amesema sensa hiyo ilianza Septemba 2024 na itakamilika mwaka huu.
“Hadi sasa tumekamilisha mifumo ya ikolojia mitano kati ya tisa, ikiwemo Katavi-Rukwa, Ruaha-Rungwa, Nyerere-Selous-Mikumi, West Kilimanjaro-Lake Natron, na Mkomazi, ambayo ni asilimia 65 ya kazi yote,” amesema.
Amesema kuwa sensa inafanywa kwa kutumia ndege zinazotumiwa na wataalamu walio ndani kuhesabu wanyama pori.
Amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya Sh4 bilioni kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo, na hadi sasa wameshatumia Sh2.7 bilioni.
Mtafiti Mkuu wa Kitengo cha Sensa ya Wanyama Pori kutoka Tawiri, Dk Hamza Kija amesema kuwa kwa awamu hii wanazingatia sensa ya wanyama aina tano ambao ni tembo, nyati, pofu, twiga na pundamilia.
“Lengo ni kupata idadi sahihi ya wanyama hawa ili kusaidia katika utengenezaji wa sera na uboreshaji wa mifumo yao ya ikolojia kwa lengo la kuwalinda, na kuhakikisha wapo siku zote.
“Pia kwa hatima ya utalii wetu na uchumi wa nchi kwa ujumla,” amesema.
Dk Kija amesema tangu kuanza kwa sensa ya wanyama pori nchini mwaka 1987 mwaka huu ni awamu ya 23.