Sh240 bilioni kujenga shule 23 za ghorofa Zanzibar

Sh240 bilioni kujenga shule 23 za ghorofa Zanzibar

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesaini mkataba na Benki ya CRDB kwa ajili ya kupata mkopo wa bei nafuu wa Euro milioni 79 (takribani Sh240 bilioni), zitakazotumika katika ujenzi wa shule 23 za ghorofa za msingi na sekondari.

Utiaji saini huo umefanyika leo Mei 21, 2025 kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ukishuhudiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Fedha hizo zitatolewa na Taasisi ya Deutsche Mark ya nchini Spain ambayo inatoa asilimia 85 na Benki ya CRDB asilimia 15 huku usimamizi wote ukifanywa na CRDB.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Mwinyi amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya Zanzibar sasa inaweza kukopa fedha kutoka nje ya nchi kupitia benki za ndani akifafanua kuwa CRDB imeonyesha njia kuwa wanaweza.

“Tangu Mapinduzi njia za kupata fedha ya miradi ya maendeleo zilikuwa za aina mbili, ama zitokane na bajeti yetu ya Serikali au fedha hizo zitokane na mkopo uliodhaminiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hii inatuonyesha kwamba tunaweza kukopa kutoka taasisi za nje kupitia benki za ndani. Napenda nichukue fursa hii kuwashukuru CRDB kuwa wa kwanza katika ushirikiano huu. Nyinyi ni wadau muhimu sana na tutaendelea kushirikiana nanyi kukamilisha miradi mingi ya maendeleo hapa Zanzibar,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema mkopo huo utasaidia kujenga shule 23 za kisasa za msingi na sekondari na kupunguza changamoto ya vyumba vya madarasa katika kisiwa hicho.

Mbali na hilo, amesema kupitia utaratibu wa hatifungani inayofuata misingi ya dini ya Kiislamu (Sukuk) na mikopo ya namna hiyo, utasaidia kufanya miradi mikubwa akitaja miradi mingine mitano ambayo itatekelezwa kupitia utaratibu huo.

Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa bandari ya Mangapwani, miradi ya afya – vituo vidogo zikiwemo hospitali za mikoa na rufaa – na kituo cha umahiri cha matibabu ya saratani.

Miradi mingine inajumuisha ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa Afcon, ambao utahusisha ujenzi wa hoteli za nyota tano na hospitali kulingana na masharti ya waandaaji.

Utekelezaji wa miradi hii utahitaji Dola za Marekani milioni 180 (takribani Sh483.343 bilioni), pamoja na ujenzi wa barabara za kimkakati.

Kiongozi huyo ametumia fursa hiyo kuwapa salamu wanaodai nchi inakopa kupita uwezo wake, akisema bado ina uwezo wa kukopa kwani uwiano katika ukuaji wa pato la taifa nchi zinazoendelea haipaswi kuvuka asilimia 50 na kwa sasa Zanzibar ipo katika asilimia 17.

“Bado tuna uwezo mkubwa wa kukopa, kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), tupo katika asilimia 17, kwa hiyo wale wanaosema sema huko niwape salamu kwamba tutaendelea kukopa na uwezo tunao,” amesema.

Katika kulifafanua zaidi jambo hilo, Dk Mwinyi amesema SMZ ina akaunti maalumu kwa ajili ya madeni ambao kila mwezi wanaweka Dola za Marekani 10 milioni (Sh26.975 bilioni), hivyo kwa mwaka mfuko huo unakuwa na Dola za Marekani 120 milioni sawa na Sh322.228 bilioni.

Akizungumzia mkopo waliopewa amesema ni wa miaka mitano na kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti hiyo wana uwezo wa kulipa kwa kipindi cha miezi sita pekee.

“Kuna watu wanasema anakopa sana, lakini ndugu zangu kukopa kuna kanuni zake, hatuwezi kwenda hivi hivi, bado uwezo tunao na tutaendelea kukopa,” amesema.

Pia, ametumia fursa hiyo kuzitaka benki kupunguza mlolongo mkubwa wanapoomba mikopo kama hiyo kwani tayari wameshaonyesha uwezo wa kulipa.

 “Tukitaka mkopo basi miezi miwili mtupe badala ya kutumia muda mrefu msiwe na shaka, mfuko wetu unazidi kutuna.”

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Nsekela amesema Zanzibar imekuwa mdau mkubwa katika kushirikiana na benki hiyo kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mikopo ya wajasiriamali wadogo ambayo haina riba.

“Tunajivunia kuwa mshirika mkubwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wameonyesha imani kubwa na sisi tutaendelea kuilinda imani hiyo kuhakikisha kwa pamoja tunaleta maendeleo makubwa,” amesema.

Kwa mujibu wa Nsekela, tangu benki hiyo ianze kushirikiana na SMZ tayari imeshatoa Sh470 bilioni akisema hicho sio kiwango kidogo cha fedha.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa amesema hadi kufikia Januari 2026, shule hizo zitakuwa zimeanza kujengwa na watahakikisha kila sehemu inanufaika na mpango huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *