Sh169 bilioni kuongeza vituo vya saratani kwa teknolojia ya nyuklia

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali zote mbili zimeandaa mpango wa kuongeza vituo vya uchunguzi na matibabu ya saratani kwa kutumia teknolojia ya nyuklia wenye thamani ya Euro 59 (Sh169.872 bilioni).

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Novemba 11 2024 kupitia hotuba yake iliyosomwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alipomwakilisha wakati wa kuzindua ofisi na maabara za Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (Taec) Zanzibar.

“Kupitia mpango huu, tumedhamiria kuongeza uwezo vituo vya Ocean Road, Dar es Salaam na Bugando, Mwanza pamoja na kuanzisha vituo vipya vinne katika hospitali za Benjamini Mkapa Dodoma, KCMC Moshi, Mnazi Mmoja Zanzibar na Hospitali ya Rufaa Mbeya,” amesema Rais Samia.

Amesema ujenzi wa benki kwa ajili ya kuwekea vifaa vya nyuklia umeanza katika hospitali za Benjamini Mkapa Dodoma na KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro, mikakati hiyo pia inaendelea katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar na eneo la Binguni pamoja na Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Amesema kukamilika kwa mpango huo kutaongeza huduma za matibabu ya saratani kwa kutumia teknolojia ya nyuklia na nchi itakuwa na vituo sita vya Serikali katika kanda zote muhimu nchini.

“Kuwepo kwa kituo hiki kutaleta manufaa makubwa katika nchi yetu hasa katika matumizi ya teknolojia ya nyuklia,” amesema Rais Samia. 

Amesema sehemu kubwa ya matumizi ya teknolojia ya nyuklia yapo katika sekta ya afya hasa kwenye uchunguzi na matibabu ya saratani, hivyo vituo vya saratani nchini ni wanufaika wakubwa wa teknolojia hiyo.

  “Nitumie fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomu (IAEA) na wadau wengine wa maendeleo kwa kusaidia Tanzania katika kuimarisha miundombinu, vifaa na utaalamu unaohitajika katika utafiti, ubunifu, udhibiti na matumizi salama ya mionzi na teknolojia ya nyuklia,” amesema Rais Samia.

 Amesema kutokana na uhaba mkubwa wa wataalamu wa sayansi na teknolojia ya nyuklia nchini, Wizara imeanzisha dirisha la ufadhili kupitia ‘Samia Scholarship Extended’ ili kuwezesha vijana wa Kitanzania kusoma shahada za umahiri za masuala ya sayansi na teknolojia ya nyuklia katika vyuo bora duniani.

 “Pamoja na mafanikio ambayo tumeyapata, ninatambua kuwa Taec ina changamoto mbalimbali ikiwamo ya uhaba wa watumishi pamoja na ufinyu wa bajeti ya kuanzisha miradi mikubwa ya teknolojia ya nyuklia nchini. “Niwahakikishie kuwa, Serikali zote mbili zitajitahidi kushirikiana katika kuongeza bajeti na nafasi za ajira katika tume hii kwa kadiri uwezo wetu wa kifedha utakavyoruhusu,” amesema Samia.

 Mkurugenzi Mkuu Taec, Profesa Najat Mohammed amesema jengo hilo limegharimu Sh3 bilioni na limejumuisha ofisi 17 na maabara tano.

Amesema jengo hilo litaongeza tija katika utekelezaji wa sera ya Taifa na teknolojia ya nyuklia ya mwaka 2013 na kuongeza biashara kwa wananchi kisiwani hapa ili kuendeleza biashara.

“Hii itasaidia pia kuhamasisha matumizi salama ya nyuklia kwa kuboresha mifumo juu ya matumizi  salama ya nyuklia na ubora wa vipimo vya mionzi hiyo,” amesema Profesa Mohammed.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taec, Profesa Joseph Msambichaka amesema Serikali imefanikiwa kuongeza eneo la ujenzi huo na kuboresha miundombinu.

Waziri wa Afya Zanzibar, Nassoro Ahmed Mazrui amesema maabara hizo mo zitasaidia sana katika sekta ya afya inayotarajiwa kuwa na kituo cha saratani.

“Wizara ya Afya tutakuwa mdau mkubwa wa maabara hizi kwani kwa sasa tupo kwenye mchakato wa kujenga kituo cha saratani, Hospitali ya Rufaa Binguni na hospitali nyingine ambazo zitakuwa na X-Ray, CT Scan na MRI,” amesema.

Naibu Waziri ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga amesema wizara hiyo inathamini mchango wa tume hiyo katika sayansi na teknolojia kwa kuweka vifaa vya kisasa kudhibiti mionzi hiyo na kuongeza uzalishaji.