
Musoma. Mamlaka za serikali za mitaa mkoani Mara zimetumia zaidi ya Sh130.3 milioni kulipia malimbikizo ya michango ya watumishi wa kada za watendaji wa kata, madereva na walinzi, ambayo haikuwasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kati ya mwaka 1994 hadi 2004.
Malipo hayo yamefanyika katika mwaka wa fedha 2024/25, huku kwa mwaka ujao wa fedha 2025/26, mamlaka hizo zikiwa zimetenga zaidi ya Sh234.8 milioni kwa ajili ya kuendelea kulipa deni hilo la michango.
Takwimu hizo zimetolewa leo Alhamisi Mei Mosi 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika kimkoa mjini Musoma.
Mtambi alibainisha kuwa serikali ya mkoa itaendelea kuzisimamia mamlaka hizo ili kuhakikisha michango yote ya wafanyakazi inawasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
“Michango ya watumishi wa kada hizo haikuwasilishwa kwa kipindi kirefu, jambo ambalo limekuwa kero kwa wahusika. Natoa hakikisho kuwa kila mtumishi atapata haki yake, kwa kuwa ni hitaji la kisheria na utumishi wa umma,” amesema Mtambi.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa watumishi wa kada zote, ambao ni msingi wa uendeshaji na maendeleo ya Taifa.
Katika kutambua umuhimu wa haki za watumishi, Mtambi amesema kuwa Serikali Kuu imetoa zaidi ya Sh2.2 bilioni kwa ajili ya kulipa posho za likizo kwa mwaka 2024/25, pamoja na Sh2.5 bilioni kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya mishahara kwa kipindi hichohicho.
Vilevile, amewataka watumishi kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwa kuhakikisha wamejiandikisha kupiga kura.
“Nawakumbusha ambao hawajajiandikisha au wanahitaji kurekebisha taarifa zao, wafanye hivyo kabla ya Mei 7 mwaka huu, kwani shughuli ya uboreshaji inaendelea mkoani kwetu,” ameeleza.
Awali, akisoma risala ya wafanyakazi, Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Mkoa wa Mara, Grace Mgonolwa ameitaka Serikali kutoa maagizo kwa mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha michango ya watumishi wa kada hizo inawasilishwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati.
Ameeleza kuwa kutowasilishwa kwa michango hiyo kumesababisha usumbufu mkubwa, hasa kwa watumishi waliostaafu, hivyo ni muhimu hatua zichukuliwe ili kuhakikisha wanapata stahiki zao.
Aidha, Mgonolwa aliitaka Serikali kuangalia suala la malipo ya nauli kwa watumishi wanaohamishwa vituo vya kazi, hasa walioko mijini, akieleza kuwa baadhi yao hawalipwi licha ya kuwa ni haki yao kisheria.