
Rungwe. Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya itatumia zaidi ya Sh10 bilioni kwa ajili mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya kukusanyia na kuhifadhi zao la parachichi.
Mradi huo umeanza kutekelezwa katika Kijiji cha Nkuga kilichopo katika Kata ya Nkuga wilayani humo, sambamba na ujenzi wa viwanda vidogo vidogo vya kuongezea thamani zao hilo.
Hatua hiyo imetajwa kuwa mwarobaini kwa wakulima kuepuka hasara inayojitokeza katika kila msimu, licha ya Serikali kuweka mikakati mbalimbali ya kunusuru zao hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Februari 22, 2025, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Mpokigwa Mwankuga amesema msimu huu wakulima walizalisha kwa tija lakini changamoto imekuwa ni masoko ya uhakika.
“Msimu huu soko la parachichi sio zuri, licha ya mwitikio mkubwa kwa wakulima kuzalisha kwa wingi, Serikali imeweka mikakati kuona namna gani linakuwa na tija hususani uhakika wa masoko ndani na nje,” amesema.
Mpokigwa amesema miongoni mwa mikakati ni kuja na suluhisho la ujenzi wa miundombinu hiyo, sambamba na kuongeza thamani ya zao hilo ili kuwasaidia wakulima kuondokana na hasara ya gharama ya uzalishaji.
“Utekelezaji wa mradi uko katika hatua za awali kikubwa tunaishukuru serikali kwa kuona njia mbadala ya kuongeza thamani zao la parachichi hususani miundombinu rafiki ya kuhifadhi kabla ya kuingiza sokoni,” amesema.
Ameongeza kuwa mpango huo utasaidia wakulima kuuza zao hilo kwa bei nzuri elekezi ya Serikali, tofauti na sasa wanunuzi wanajipopangia bei mashambani.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo Wilaya ya Rungwe, Adam Salum amesema kwa msimu huu uzalishaji umepungua kutoka kilo 5.8 milioni mpaka kilo 4.3 milioni na kwamba uzalishaji umeshuka.
Amesema kwa upande wa bei elekezi ya Serikali, awali ilikuwa Sh2, 000 kwa kilo moja baada ya kuona bado soko si zuri, ikashuka na kufikia Sh1,000 kwa kilo, lakini bado soko lake si zuri.
Salum amesema kutokana na changamoto hiyo, Serikali inaendelea kuangalia sababu za kuyumba kwa soko la zao la parachichi.
Mkulima wa zao hilo, Ipyana Mwalukasa amesema msimu huu zao hilo limeporomoka na kuwalazimu kuuza Sh800 mpaka Sh600 kwa kilo, licha ya bei elekezi ya Sh1, 000 kufuatia uzalishaji kuwa mkubwa lakini masoko hakuna.
Amesema shida haipo upande wa Serikali, bali ni upande wa wanunuzi kukwama usafirishaji kwenda mataifa mbalimbali kwenye masoko, jambo ambalo kila mmoja linamgusa kwa namna fulani.
“Kimsingi hali sio nzuri kabisa, masoko hakuna na hakuna wa kumlaumu, Serikali haipendi kukosa mapato, kikubwa tunaomba ione njia mbadala ya kutusaidia ili kuepuka hasara kwani asilimia kubwa matunda yanaharibikia mashambani,” amesema.
Mei 11, 2024, Mkurugenzi wa Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Enock Nyasebwa alieleza kuanza kwa mpango wa kuweka vigezo ili kuhakikisha miche inayopandwa inakidhi vigezo, lengo likiwa ni kuongeza thamani na ubora wa zao hilo ili kufanya vizuri kwenye soko la kimataifa na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.
Nyasebwa alitoa kauli hiyo wakati akitoa ufafanuzi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kiwira, Wilaya ya Rungwe mkoani hapa.