
Hatua ya Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutangaza kuanza mchakato wa ujenzi wa Reli ya SGR Mijini (Commuter Rail Network – CRN) kwa Jiji la Dar es Salaam na Dodoma ni ishara ya uamuzi sahihi unaoendana na mahitaji ya sasa ya maendeleo.
Kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, kwamba usanifu wa awali na upembuzi yakinifu wa mradi huo umekamilika, ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati ambao unawezesha umma kutumia treni za kasi na za kisasa katika safari za ndani ya miji hiyo.
Kwa muda mrefu, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakikabiliana na changamoto sugu ya msongamano wa magari, hasa wakati wa asubuhi na jioni.
Baadaye ulianza mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) ambao mpaka sasa haujafanya vizuri, licha ya kuanza takribani miaka 10 iliyopita.
Kuwapo kwa reli hii ya mijini kutakuwa mkombozi mkubwa, kwani itarahisisha usafiri wa kila siku wa maelfu ya wakazi, kupunguza matumizi ya mafuta, na kuongeza ufanisi wa uzalishaji kutokana na kupungua kwa muda unaopotea barabarani.
Ni dhahiri kuwa uwekezaji wa aina hii hauhitaji tu dhamira, bali pia usimamizi madhubuti.
Treni za mijini tofauti na mabasi ni njia ya usafiri inayotunza muda, haina mwingiliano na magari mengine, na inaweza kusafirisha abiria wengi kwa wakati mmoja.
Katika nchi zilizoendelea, mfumo huu wa usafiri umekuwa uti wa mgongo wa shughuli za kila siku za kiuchumi na kijamii mijini na reli zinatandazwa chini ya ardhi, juu ya ardhi na angani.
Taarifa kuwa Serikali itatekeleza mradi huo kwa ubia na sekta binafsi (PPP) ni jambo la kupongezwa.
Ushirikiano wa namna hii unaweza kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa bila kuiweka Serikali kwenye mzigo mkubwa wa kifedha.
Aidha, ushiriki wa sekta binafsi unaweza kuongeza ubunifu, ushindani wa huduma, na ufanisi unaohakikisha huduma bora kwa wananchi tofauti na inavyokuwa pale huduma za kibiashara zinapotolewa na sekta ya umma.
Mbali na Dar es Salaam, hatua ya kuifikiria pia Dodoma kama mji mwingine wa kunufaika na reli ya mijini ni ishara kuwa Serikali inaangalia usafiri wa mijini kama sekta pana inayopaswa kufikiriwa kwa mtazamo wa kitaifa.
Hata hivyo, tunaamini kuwa huu ni wakati mwafaka pia wa kuyatazama majiji kama Arusha, Mwanza na Mbeya ambayo nayo yanakua kwa kasi na yana uhitaji mkubwa wa mifumo ya usafiri wa umma thabiti.
Wakati Tanzania inazidi kusonga mbele katika kujenga miundombinu ya kisasa, ni muhimu kuhakikisha kuwa miradi kama hii inatekelezwa kwa weledi, kwa uwazi, na kwa kushirikisha wananchi.
Aidha, ni muhimu kuhakikisha kuwa huduma zitakazotolewa zinakuwa za viwango vya juu, salama, nafuu, na zinazowahusu watu wote, wakiwemo wenye ulemavu, wazee, wanawake na vijana.
Kwa kifupi, mpango huu wa CRN ni fursa ya kihistoria ya kubadili sura ya usafiri wa mijini nchini.
Tunaihimiza Serikali kutekeleza mradi huu kwa haraka, lakini kwa uangalifu mkubwa, huku ikiweka misingi imara ya usimamizi, uendelevu na ubora wa huduma.
Kama tukifanikiwa, Tanzania inaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine za Afrika katika kujenga miji yenye usafiri wa kisasa, bora na wa kuaminika.