Serikali yazindua Bodi ya kima cha chini cha mshahara

Dodoma. Serikali imeagiza bodi ya kima cha chini cha mshahara kuwasilisha mapendekezo ya viwango vya mishahara kwa kuzingatia hali halisi ya maisha na kuepusha migogoro makazini.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene aliyesema mapendekezo hayo yanalenga kuwa na kiwango kitakachosaidia morali ya wafanyakazi, tija na uzalishaji.

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha wizara hiyo, kinaeleza kuwa Waziri Simbachawene ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akizindua bodi ya kima cha chini cha mshahara katika utumishi wa umma.

Agizo la Waziri linakuja katika kipindi ambacho kumekuwa na malalamiko kuhusu kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma, lakini kilio kikubwa kikiwa kwa sekta binafsi.

Ripoti iliyochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa watu 1,996,555 kati ya 3,717,980 walio katika ajira wanalipwa kati ya Sh0 hadi 499,999 wakati wanaolipwa mshahara wa Sh700,000 ni asilimia 27.2 pekee.

“Kima cha chini cha mshahara kisichozingatia hali halisi ya uchumi ni hatari katika maendeleo ya nchi hasa kutokana na ukweli kwamba kunaweza kusababisha kutokea kwa mfumuko wa bei, na kuongeza gharama za uendeshaji,” amesema Simbachawene.

Kwa mujibu wa waziri, bodi hiyo ina jukumu la kufanya uchunguzi na kupendekeza kwa waziri mwenye dhamana na masuala ya utumishi wa umma kuhusu kima cha chini cha mshahara katika sekta ya umma, hivyo katika kutekeleza majukumu hayo, ina wajibu wa kuzingatia masilahi na mustakabali wa uchumi wa nchi wakati wa kutoa mapendekezo stahiki.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Utumishi ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Taasisi, Nolasco Kipanda amesema mbali na uzinduzi wa bodi hiyo, wajumbe watapatiwa mafunzo kwa ajili ya kujengewa uwezo na kupata uelewa kuhusu majukumu ya upangaji wa kima cha chini cha mshahara katika utumishi wa umma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo  katika utumishi wa umma, Mathias Kabunduguru amemuahidi waziri kuwa watatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na malengo yaliyokusudiwa katika kupendekeza na kutoa ushauri kwa ustawi wa nchi.

Bodi hiyo imeanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 35(1) cha Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya mwaka 2004 na marekebisho yake katika kifungu cha 14(b) cha Sheria ya Ajira na Kazi Na. 24 ya mwaka 2015.

Baada ya kupitishwa na Bunge Julai 2015, Serikali ilianzisha bodi mbili ikiwemo moja kwa ajili ya sekta binafsi na nyingine kwa ajili ya sekta ya umma.