Serikali yawekeza Sh55.7 bilioni kiwanda cha viuadudu Kibaha

Kibaha. Serikali imewekeza dola milioni 22.3 (Sh 55.7 bilioni) kwenye kiwanda cha kuzalisha viuadudu cha Tanzania Biotech Product (TPBL) kinachoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Cuba na Tanzania.

Leo Machi 5, 2025 Rais wa Bunge la Cuba, Esteban Lazo Hernandez amekitembelea kiwanda hicho kilichopo Kibaha mkoani Pwani  kushuhudia uzalishaji wake, akieleza kwamba kinakwenda kuwa mkombozi katika vita ya kutokomeza malaria nchini.

Hernandez katika ziara yake ameeleza namna kiwanda hicho kinavyotumia teknolojia pekee kutoka Cuba, akibainisha kwamba kipo nchini Tanzania kutokana na ushirikiano wa nchi hizo mbili, ulioasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Cuba, Fidel Castro.

“Kuanzishwa kwa kiwanda hiki ni mwendelezo wa kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Cuba katika maeneo tofauti ikiwamo ya uchumi na afya na kuendeleza uhusiano wa kihistoria uliojengwa na viongozi hao.

“Kiwanda hiki ni moja ya maeneo muhimu katika uhusiano huu kwa kuwa ni sehemu ya teknolojia inayopatikana Cuba pekee, Cuba inaunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya malaria,” amesema.

Amesema umuhimu mkubwa wa kiwanda hicho cha viuatilifu, viuadudu na mbolea hai ni mapambano dhidi malaria.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Nicholaus Shombe amesema kiwanda hicho kinachangia kwa kiasi kikubwa katika kutokomeza malaria nchini.

 Amesema Serikali ya Tanzania imewekeza dola milioni 22.3 katika kiwanda hicho ambacho kinaendeshwa kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Serikali ya Cuba.

 “Tuna wataalamu kutoka Cuba ambao tunashirikiana nao, wameleta teknolojia ya kuzalisha na namna ya kuendesha,” amesema.

Amesema Serikali katika mapambano ya malaria, mwaka huu imeshatoa Sh4.5 bilioni ambazo zote zimetumika kuzalisha dawa ya kutokomeza malaria ambayo imesambazwa mwenye halmashauri mbalimbali nchini.

Amebainisha kwamba dawa hiyo si tu kwa ajili ya matibabu bali kuzuia kabisa maambukizi ya ugonjwa wa malaria ambao ni gharama kuutibu.

Mbali na malaria, Shombe amesema pia kiwanda hicho ambacho ni kikubwa kwa Afrika katika uzalishaji wa viuadudu, viuatilifu na mbolea hai kimezalisha dawa ya mazao isiyo na sumu.

“Mkulima akiitumia anapata mazao ambayo hayana sumu na thamani yake sokoni inaongezeka. Tunafahamu hivi sasa kumekuwa na ongezo na matukio ya magonjwa kama kansa, wanasayansi wakiyahusisha na kemikali, ili kutokomeza hilo  tunakwenda kuzalisha ‘fertilizer’ ambayo mkulima akitumia hivi viuatilifu anapata zao lisilokuwa na sumu,” amesema.

Amesema kiwanda hicho kinataka kufikia kiwango cha juu cha uzalishaji hadi wa lita milioni sita za viuadudu na viuatilifu lakini kwa sasa uzalishaji ni  lita milioni moja na laki mbili,”

Amesema  hivi karibuni pia wataanza kutengeneza mbolea hai ambayo ni miongoni mwa bidhaa 10 zinazotarajiwa kuzalishwa na kiwanda hicho.

Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya viwanda na Biashara, Dk Suleiman Serera amesema lengo la Serikali ni kutokomeza kabisa malaria.

Akizungumzia umuhimu wa kiwanda hicho kwa mwananchi wa kawaida, Dk Serera amesema kwanza kinatoa fursa kwa wananchi kuwauzia wadudu hai wa mashambani, ambao kiwanda kitawatumia kutengeneza mbolea hai.

“Pia tutafanya ushirikiano pamoja na wakulima ili wataalamu wetu wawe wanakwenda mashamba ya jirani kutoa elimu,” amesema na kuongeza.

“Hata mbolea hai inayotengenezwa katika kiwanda hiki haina kemikali, wakulima wanapoitumia inakuja na matokeo chanya ya kiafya kwa wananchi,” amesema.

Amesema magonjwa mengi yasiyo ya kuambukiza ambayo huwapata watu wengi, mengi yanachagizwa na vyakula vyenye dawa zenye kemikali nyingi.

Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole amesema jitihada kubwa za Serikali ni kupambana na malaria na kuokoa watu wake.

 “Uwepo wa kiwanda hiki Tanzania kuna manufaa makubwa katika kuboresha afya za Watanzania, tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambazo zimewezesha viuadudu kuzalishwa na kusambazwa kote nchi,” amesema.