Serikali yawaonya wanaotaka kufanya fujo uchaguzi mkuu

Dodoma. Serikali ya Tanzania imewaonya watu waliojipanga kuleta fujo, kujihusisha na rushwa ama kuleta sitofahamu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kuwa ipo macho na haitatoa mwanya wa kufanyika hila hizo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 9, 2025 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mwera (CCM), Zahoro Mohamed Ally.

Mbunge huyo amehoji Serikali imejipangaje kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2025 ukizingatia kuna upungufu wa watumishi na vitendea kazi.

Akijibu swali hilo, Simbachawene amesema Serikali imejipanga na kudhamiria kuwa na uchaguzi wa huru na wa haki ambao viongozi watachagua kwa uwezo wao wa kuongoza na kuwahudumia wananchi, na sio kwa kuwarubuni wapiga kura kwa rushwa.

“Katika kutimiza azma hii ya Serikali, Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) imejipanga kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kutoa elimu kwa umma kwa kutumia njia mbalimbali kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi, kufuatilia nyendo za wagombea na wapambe wao kwa lengo la kuzuia vitendo vya rushwa,”amesema.

Serikali yatoa onyo wanaotaka kuzuia uchaguzi

Simbachawene amesema pia wamejipanga kukusanya taarifa za kiitelejensia kuhusu vyanzo vya mapato ya wagombea, wapambe na vyama vya siasa ili kudhibiti fedha haramu.

Pia amesema wamejipanga kuchunguza na kuwachukulia hatua za kisheria wagombea watakaojihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2025.

Aidha Simbachawene amesema mwaka 2023/24 Serikali iliiwezesha Takukuru kuajiri watumishi 350, kununua magari 178 na vitendea kazi vingine ili kuimarisha utendaji wa kazi katika ofisi za mikoa na wilaya.

Katika swali la nyongeza, Zahoro ameuliza,  “Kwa sababu Serikali imesema katika mwaka 2023/24 imeajiri 3,050 je, idadi hii ndio hitajika ama kuna idadi inahitajika ama nini kinafanyika?

Kuhusu kuwapo kwa dalili za uvunjifu wa amani, lugha na kejeli na mambo mengi mbunge huyo ameiomba Serikali iliambie Bunge wamejipangaje kuhakikisha uchaguzi  unakuwa salama, huru, haki na hakuna mtu anayeweza kuzuia uchaguzi kwa mujibu wa Katiba.

Akijibu swali hilo, Simbachawene amesema Serikali tangu iingie madarakani imeweka nguvu kubwa katika kupambana na rushwa na kuwa wamepata vifaa vya kazi ambavyo havijawahi kuwapo tangu chombo hicho kimeanzishwa.

“Takukuru wamepatiwa magari 178 hiyo itatusaidia katika kupambana katika ngazi ya wilaya. Lakini tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya sita hadi 2025, tumeweza kuongeza watumishi 1,190. Tunaamini hawa sasa wanatosha,” amesema.

Amesema kila ofisi ya wilaya sasa ina watumishi wa Takukuru kati ya watano hadi 15 , hivyo wanaamini wanaweza kupambana na rushwa ama kutoa elimu kwa Watanzania kwa kuwa ndio sehemu wanaojikita nayo.

Amesema lengo la kutoa elimu ni kuhakikisha wananchi wanajua madhara ya rushwa.

Kuhusu rushwa katika uchaguzi, Simbachawene amesema Tanzania ina uzoefu mkubwa katika kushughulika na uchaguzi kwa sababu  wameshafanya takribani chaguzi kuu saba hivyo  kuwa mwalimu wa demokrasia katika ukanda wa kati.

“Ni kuhakikishie kwa wale ambao wamejiandaa kuleta fujo ama mambo ya sintofahamu kwa jamii, Serikali hata siku moja huwa haipumziki wala hakuna gap (mwanya), Serikali ipo na hata kama tupo hapa na wengine wako wapi lakini ipo.

“Vyombo vyetu katika kusimamia sheria huwa vina ushirikiano hakuna mahali ambapo kutakuwa na upungufu wa watu wanaosimamia sheria. Serikali imejipanga katika kusimamia uchaguzi wa mwaka 2025, kama ambavyo tumeshughulikia nyingine kwa mafanikio makubwa,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *