Serikali yatenga Sh45.1 bilioni kudhibiti wanyamapori

Dares Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetenga Sh45.1 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kutekeleza mikakati na mipango ya kudhibiti migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika maeneo mbalimbali nchini.

Hiyo ni sehemu ya juhudi za kudumisha usalama kwa jamii zinazopakana na maeneo ya uhifadhi.

Ofisa Mkuu wa Wanyamapori, Anthonia Raphael, ameeleza hayo jana Novemba 8, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa akizungumza na Mwananchi kando ya majadiliano yaliyoandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).

Anthonia amesema: “Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya Sh45.1 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mikakati na mipango iliyowekwa kudhibiti migongano hii.”

Aidha, Anthonia aliongeza kuwa hadi Oktoba 2024, kiasi cha Sh1.2 bilioni kimetolewa kwa wananchi 4,142 katika wilaya 14 ikiwemo Tunduru na Namtumbo kama fidia kwa walioathirika na wanyamapori.

“Wizara inashirikiana na wadau mbalimbali kufanya mapitio ya Mkakati wa Taifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori (2020-2024) ili kuendana na changamoto za sasa,” amesema Anthonia.

Kulingana na Anthonia, katika mwaka wa fedha uliopita wa 2023/2024, mpango wa kifuta jasho na kifuta machozi ulitoa Sh3.1 bilioni kwa wananchi 14,959 waliopata madhara kutokana na wanyamapori kwenye halmashauri 53 za wilaya, zikiwemo Liwale, Nachingwea, Namtumbo, Tunduru, Tandahimba, Newala, Morogoro Vijijini na Mvomero.

Pamoja na mikakati hiyo, Wizara ya Maliasili na Utalii inapanga kuimarisha utekelezaji wa mkakati wa kuokoa shoroba za wanyamapori (2022-2026) na kuboresha mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi.

Raphael amesisitiza kuwa ushirikiano na wadau wa uhifadhi na Wizara za Kisekta unalenga kuhakikisha mikakati hiyo inatekelezwa kwa ufanisi ili kupunguza athari za migongano kwa jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dk Fortunata Msofe, ameeleza kuwa serikali inalenga kushirikiana na jamii ili kudhibiti migongano kwa kuimarisha usimamizi wa maeneo ya muingiliano na kutoa elimu kuhusu faida za uhifadhi na mbinu za kukabiliana na migongano.

“Pia kuna elimu ya mbinu za uhimilivu kwa namna ambavyo wananchi wanaweza kuendelea na shughuli zao na ufuatiliaji wa matukio,” amesema Dk Msofe.

Upande wake Mwenyekiti wa JET, Dk Ellen Otaru, aliwahimiza waandishi wa habari kutumia nafasi yao vizuri ili kuchochea mabadiliko kwa manufaa ya jamii na mazingira.

“Wanahabari wana nafasi kubwa mno katika kuleta mabadiliko na kuchangiza wadau ikiwamo serikali kuweza kuchukua hatua,” alisema Dk Otaru.

Kulingana Takwimu za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) zinaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko la matukio ya wanyamapori kuingia kwenye makazi ya watu mwaka hadi mwaka huku moja ya sababu ikiwa ni watu kujenga makazi kwenye mapito (shoroba) ya wanyamapori.

Kuwapo kwa mwingiliano huo kumekuwa kukisababisha athari kwa binadamu na wanyamapori ikiwemo kuharibiwa kwa mazao, watu kujeruhiwa, kuuawa na wanyama hao na pia kubadilika kwa tabia za wanyamapori.

Takwimu za Tawa zinaonyesha kwamba mwaka 2016/17 kulikuwa na matukio 833 ambapo mwaka 2017/18 yaliongezeka hadi kufikia 997 na mwaka uliofuata wa 2028/19 yaliongezeka zaidi hadi kufikia 1,510.

Mwaka 2019/20, matukio ya wanyama kuingia kwenye makazi ya watu yalipungua kidogo hadi kufikia 1,426, mwaka 2020/21 yalifika 1706, mwaka 2021/22 yalikuwa 2,304 na mwaka 2022/23 yalikuwa 2,817.

Majadiliano hayo yalifadhiliwa na Mradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani (BMZ).