Serikali yasisitiza majibu mazuri huduma kwa wateja Tanesco

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema wapokeaji wa simu za wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wanaopiga simu kwa ajili ya kuhitaji huduma,  wanapaswa kutoa majibu mazuri.

Amesema majibu yanayotolewa kwa wateja ndiyo yanayobeba taswira ya shirika hilo la umeme nchini, hivyo wahudumu wanapaswa kuzingatia suala hilo.

Kapinga ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 12, 2025 wakati wa hafla ya uzinduzi wa namba mpya ya huduma kwa wateja ya Tanesco ambayo ni namba 180, iliyofanyika kituo cha miito ya simu kilichopo Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam.

Amesema katika kuhakikisha hilo usimamizi wa karibu unahitajika kwa mameneja wa mikoa na maofisa huduma kwa wateja, ili kulipa taswira nzuri shirika hilo.

“Lugha na namna ya kuhudumia wateja inapaswa kuzingatiwa kwa ufanisi, Serikali haitavumilia huduma zisizokidhi vigezo kwa wateja. Kituo cha miito ya simu kinabeba taswira ya shirika hivyo atakayetenda kinyume achukuliwe hatua,” amesisitiza Kapinga.

Aidha, amesema uzinduzi wa namba hiyo ni utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ya kwamba Tanesco wanapaswa kuimarisha utoaji huduma kwa wateja.

Amesema namba hiyo mpya ya bure itawezesha Tanesco kujiimarisha kutoa huduma kwani wateja wengi zaidi watatoa taarifa za changamoto zitakazotatuliwa kwa wakati.

“Serikali imedhamiria wananchi watatuliwe matatizo yao yahusianayo na umeme kwa wakati na kwa ufanisi ili kuleta huduma bora zenye viwango,” amesema Kapinga.

Aidha, amesema kwa upande wa nishati safi ya kupikia umeme ni salama na nafuu,  hivyo wanahamasisha Watanzania kununua vifaa vya kutumia umeme ikiwemo majiko yanayotumia nishati hiyo kidogo kwa kuwa ipo ya kutosha.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Gisima Nyamo-Hanga amesema huduma ya miito ya simu ilionekana kupungua kwa kiwango cha huduma inayopatikana kwa wateja.

Amesema kutokana na hilo viongozi wa Serikali wakaelekeza kutafutiwa ufumbuzi wa malalamiko hayo, hivyo namba hiyo mpya ya 180 ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo hayo.

“Awali namba waliyokuwa wakitumia wateja kupiga walikuwa wanalipia ila namba hii mpya ni bure na ina uwezo wa kuhudumia wateja wengi kwa wakati mmoja.

“Huduma kwa wateja ni sehemu ya msingi na ndio kitu pekee kilichowezesha mashirika na kampuni nyingi duniani kuendelea kuwepo. Hivyo tutahakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji ya wapewa huduma,” amesema.

Amesema miito ya simu inapaswa kuhakikisha inapatikana kwa wakati kwa ajili ya kuhudumia wananchi bila usumbufu.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco, Balozi Zuhura Bundala amesema umeme unategemewa kuanzia nyumbani hadi viwandani hivyo upatikanaji wake ni muhimu na unapaswa uwe wa uhakika.

Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Irene Gowele, amesema huduma watakazozitoa si kwa kupokea simu tu, bali kwa kutoa huduma bora na rahisi kwa wananchi.

“Tutaendelea kuboresha huduma zetu kwa ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *