
Dodoma. Wizara ya Maliasili na Utalii imeliomba Bunge kuwaidhinishia Sh359.98 bilioni kwa mwaka 2025/26 kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbe 10, huku ikipunguza na kufuta ada zilizokuwa kero katika sekta ya utalii, ambapo sasa waongoza watalii wataingia kwenye hifadhi bila kulipa ada.
Hayo yamesemwa leo Mei 19,2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2025/26.
Mbali na hivyo, wizara hiyo imeomba Bunge kuidhinishia Sh359.98 bilioni katika mwaka 2025/2026 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele 10 huku Sh105.74 bilioni zikiombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Katika mwaka 2024/2025, Wizara hiyo iliidhinishiwa Sh348.12 bilioni kati ya fedha hizo, Sh97.24 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Dk Pindi amesema Serikali imefuta malipo ya waongoza watalii (park fees) walizokuwa wakitozwa kila walipokuwa wakiingia hifadhini kuingiza wageni.
“Sasa kila mwongoza watalii mwenye leseni hai na halali hatatozwa chochote,”amesema.
Amesema pia wameanza kutekeleza punguzo la ada ya wakala wa kupandisha mlima kutoka Dola za Marekani 2,000 (Sh5.2 milioni) hadi Sh3 milioni.
Aidha, Dk Pindi amesema Wizara imeanza kutekeleza punguzo la gharama ya leseni ya waongoza watalii (TTBL) kutoka Dola za Marekani 50 (Sh130,000) hadi Sh35,000 tu kwa mwaka.
“Wizara na Serikali kwa ujumla itaendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi katika kuongeza ufanisi wa sekta za uhifadhi na utalii kupitia vikao vya kisekta chini ya TNBC pamoja na mikutano ya mara kwa mara na wadau,”amesema.
Dk Pindi amesema wizara imefanikiwa kuanza kutekeleza hatua madhubuti na za kimkakati za kusaidia sekta binafsi iweze kukua katika sekta ya utalii kwa kupunguza na kuondoa tozo na kero zilizokuwa zinawakwaza wadau.
Amesema wizara imefanya mabadiliko ya viwango vya ada ya leseni ya Biashara za Utalii (TTBL) kwa ajili ya wawekezaji wazawa wa huduma za malazi zilizopangwa katika daraja za ubora na zile ambazo hazijapangwa katika daraja kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji.
Dk Pindi amezitaja ada nyingine zilizopungua ni daraja la nyota tano kutoka Dola za Marekani 2,500 hadi Dola1,500 (Sh6.5 milioni hadi Sh3.9 milioni) daraja la nyota nne kutoka Dola 2,000 hadi Dola 1000 (Sh5.2 milioni hadi Sh2.6 milioni).
Nyingine zilizopungua ni daraja la nyota tatu kutoka Dola 1,500 hadi Dola 500 (Sh3.9 milioni hadi Sh1.3 milioni), daraja la nyota mbili kutoka Dola 1,200 hadi Dola 300 (Sh3.12 milioni hadi Sh780,000) na daraja la nyota moja kutoka Dola 1,000 hadi Dola 200 (Sh2.6 milioni hadi Sh520,000).
Amesema gharama hizo hivi sasa zinalipwa kwa shilingi ya Tanzania. Kwa upande wa ujangili, Dk Pindi amesema Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF), umefanya operesheni za kuzuia ujangili zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 45, vipande 51 vya meno ya tembo, magamba 114 ya kakakuona, kobe hai 11 na nyara zingine.
Amesema vilevile, jumla ya silaha 13 zimekamatwa katika mwaka 2024/25 ambazo ni AK 47 moja , Rifle nane, Shotgun tatu na Gobore moja na risasi 65 za AK 47.
Vipaumbele vya wizara
Akiwasilisha hotuba hiyo, Dk Pindi amesema wizara hiyo itatekeleza vipaumbe 10 katika mwaka 2025/26 ikiwemo kuendelea kutangaza utalii ndani na nje ya nchi , kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati na kuboresha miundombinu ya utalii na uhifadhi.
Vingine ni kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa uhifadhi na rasilimali, ufuatiliaji, utangazaji na uendeshaji wa shughuli za utalii, kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, misitu, nyuki na malikale na kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya misitu na nyuki.
Ametaja vingine ni kuendelea kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa takwimu mbalimbali, kufanya tafiti za kimkakati na kutoa huduma za ushauri zinazohusu masuala ya uhifadhi endelevu wa wanyamapori, misitu na nyuki, malikale na uendelezaji utalii.
Vingine ni kuelimisha na kuhamasisha Jamii kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori, malikale, misitu na ufugaji nyuki pamoja na kuimarisha usimamizi wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za utalii na uhifadhi.
Ametaja kipaumbele kingine ni kuandaa na kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia na kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.
Aidha, Dk Pinda amesema kuwa fedha za miradi ya maendeleo zimeelekezwa katika shughuli mbalimbali za Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) ambapo Sh17.0 bilioni zimetengwa.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) limetengewa Sh18.48 bilioni kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa jengo la “control room” kubwa kwa ajili ya ufuatiliaji wa mwenendo wa magari ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Nyingine ni ujenzi wa makumbusho ya marais, Dodoma ambao umetengewa Sh1 bilioni na mradi wa uendelezaji wa utalii wa mikutano na matukio ambao utatumia Sh908.97 milioni.
Dk Pindi amesema fedha Sh32.25 bilioni zitakwenda katika mradi wa kuimarisha usimamizi wa mashamba ya miti ya Serikali na uhifadhi wa misitu ya mikoko.
Pia, amesema mradi wa usimamizi wa mifumo ya chakula, matumizi bora ya ardhi na urejeshaji wa uoto wa asili tanzania ambao unafadhilia na mfuko wa mazingira wa dunia utatumia Sh3.66 bilioni.
Dk Pindi amesema mradi wa kuwezesha mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki (BEVAC) ambao utatumia Sh1.84 bilioni.
Mradi wa kujenga uwezo wa taasisi na mafunzo ya misitu na ufugaji nyuki ambao utatumia Sh570.40 milioni huku mradi wa kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya nyara ukitumia Sh2.58 bilioni.
Miradi mingine ni mradi wa kujenga uwezo wa maeneo ya hifadhi, mapori ya akiba na kikosi dhidi ya ujangili utatumia sh1.11 bilioni na mradi wa kuendeleza utalii kusini utatumia sh18.68 bilioni.