
Dodoma. Serikali imesikia kilio cha staa wa Bongofleva, Naseeb Abdul, maarufu Diamond Platnumz cha kutengeneza Arena kwa ajili ya matamasha makubwa ya miziki baada ya Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kutenga maeneo matatu kwa ajili hiyo.
Diamond aliomba Serikali kujenga Arena wakati akiingia kwenye tuzo za muziki za ‘Trace’ zilizofanyika Februari 26, 2025 Zanzibar.
“Fikiria Arusha kunatengenezwa uwanja mwingine. Tungepata Arena na sisi ingetusaidia, hizi ‘event’ (matukio) zikifanyika nyingi zinatukuza. Wasanii wa Kitanzania tumejitahidi sana kuweka nguvu ya kisanaa ambayo inaonekana,” amesema.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Nyakaho Mahemba amesema hayo leo Ijumaa Februari 28,2025 wakati akizungumzia mafanikio na mwelekeo wa taasisi yake katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Amesema mfuko huo una viwanja katika maeneo matatu ambayo ni Mwananyamala (Dar es Salaam) na Itega na Nala (Dodoma) kwa ajili ya ujenzi wa Arena.
“Tumeshapeleka maombi kwa wafadhili mbalimbali kujenga Arena. Na tumeshapata mmoja tuko katika mazungumzo kwa ajili ya kuwekeza katika moja ya viwanja,”amesema.
Amesema iwapo kuna msanii ambaye anataka kushirikiana na Serikali kujenga maeneo hayo basi ajitokeze ili kufanya hivyo.
Aidha, amesema bajeti kwa ajili ya utoaji wa mikopo ya wasanii imeongezeka kutoka Sh1.6 bilioni mwaka 2023/24 hadi Sh3 bilioni mwaka 2025/26.
Amesema katika kipindi cha kati ya mwaka 2022, mfuko huo umetoa mikopo kwa miradi ya sanaa 389 yenye thamani ya Sh5.2 bilioni.
Mahemba amesema kiwango cha chini Sh200,000 hadi Sh100,000 ambazo hutolewa kwa msanii na mwandishi mmojammoja au kikundi ama kampuni ambapo riba yake ni asilimia tisa.
Amesema mfuko huo umesaidia kuwafanya wasanii wengi ambao baadhi walikuwa hawakopesheki kutokana na shughuli zao kutokuwa rasmi.
Mmoja wa wabunifu wa sanaa ya urembo mkoani Dodoma, Ashura Mwinyimvua ameomba mfuko huo kuongeza wigo wa elimu kwa wasanii ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.