Serikali yashtuka, yaonya ujenzi holela maeneo hatarishi

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza kuanza utekelezaji wa hatua madhubuti za mageuzi katika kukabiliana na maafa, kwa lengo la kuimarisha mifumo ya utoaji na upokeaji wa taarifa.

Imesema huo ni sehemu ya mkakati wa kudhibiti changamoto za mara kwa mara kama mafuriko na utiririshaji wa maji machafu kuelekea baharini.

Waziri Hamza ameyasema hayo wakati akisoma tangazo la Serikali lililotolewa leo Alhamisi kwenye uzinduzi wa Mkakati wa Ufuatiliaji wa Fedha katika Kukabiliana na Maafa kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2030.

Amesema mkakati huo ni nyenzo pia muhimu ya kujenga uwezo wa kitaasisi na uelewa mpana kuhusu uwekezaji unaofanywa wa kukabiliana na majanga.

Amesema pia unaainisha fursa za kuandaa programu madhubuti zitakazosaidia kupunguza athari zinazotokana na maafa.

Wafanyakazi mbalimbali walioshiriki katika uzinduzi wa mkakati wa ufuatiliaji wa fedha katika kukabiliana na maafa kwa mwaka 2025/30.

“Hatua hii imekuja wakati mwafaka, tukiwa katika mchakato wa mageuzi makubwa kwenye sekta ya kukabiliana na maafa. Lengo letu ni kuimarisha mifumo ya mawasiliano kwa wakati wa dharura kwa kushirikiana na wadau wote,” amesema.

Waziri huyo pia ameonya juu ya tabia ya baadhi ya wananchi kuendeleza ujenzi holela katika maeneo hatarishi, akibainisha kuwa baadhi ya majanga yanachangiwa na shughuli za kibinadamu.

Aidha, amewasihi madereva kuzingatia usalama kwa kuepuka mwendokasi na kushauri wananchi kuwa na bima ya mali na makazi ili waweze kupata msaada wa haraka pindi maafa yanapotokea.

Wakati huo huo, Serikali ya Zanzibar imelitambua Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuwa mshirika muhimu katika juhudi za kupunguza athari za majanga.

Waziri Hamza ameliomba shirika hilo kuendeleza ushirikiano wake kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watendaji na viongozi wa sekta husika pamoja na kusaidia upatikanaji wa vifaa na teknolojia ya kisasa.

UNDP: “Uzinduzi ni Mwanzo wa Safari Mpya ya Ustahimilivu”

Mwakilishi wa UNDP, Weynmi Omamuli, alisema Zanzibar, kama sehemu ya dunia, inakumbwa na madhara ya moja kwa moja yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na majanga ya kiasili na kuongeza kuwa mkakati huo ni hatua ya msingi kuelekea kujenga jamii inayoweza kustahimili athari hizo.

“Uzinduzi huu ni mwanzo wa sura mpya katika safari ya Zanzibar kujenga ustahimilivu dhidi ya majanga. Ni muhimu kwa sekta zote kuimarisha uratibu ili kuhakikisha jamii inalindwa,” amesema Omamuli.

Ofisa Mradi kutoka UNDP, Josephine Laswai amesema shirika hilo limeendelea kusaidia mataifa mbalimbali duniani kujenga mifumo madhubuti ya kudhibiti majanga.

Ameishauri Zanzibar kuwekeza katika mipango ya kifedha kwa kushirikiana na wadau, sambamba na kujifunza kutoka kwa nchi ambazo zimefanikiwa katika mapambano dhidi ya maafa.

“Ushirikiano wa pamoja kati ya serikali, taasisi na jamii ndio silaha kuu ya kuhakikisha maisha na mali za wananchi zinalindwa dhidi ya athari za majanga,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *