Dodoma. Ujangili wa wanyamapori Tanzania bado ni changamoto inayoilazimu Serikali kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana nayo ikiwamo kuanzisha vikosi kazi vya ardhini, majini na angani.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana amesema hayo leo Jumatatu, Machi 3, 2025 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani.
Amesema mbali na mafanikio yaliyopatikana katika uhifadhi wa wanyamapori, bado ziko changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwamo masuala ya ujangili na biashara haramu ya nyara za Serikali na misitu.
Dk Chana ametoa rai kwa Watanzania kukabiliana na biashara haramu ya nyara za Serikali na misitu.
“Bado kuna changamoto ya kuzibwa kwa shoroba kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwamo makazi ya watu. Wakati umefika sasa wa kukaa pamoja kuhakikisha tunatambua na kuziongoa shoroba,” amesema Dk Chana.

Baadhi ya askari wa wanyamapori wakiwa katika gwaride ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani.
Amesema ili kukabiliana na changamoto ya ujangili, Serikali kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua mbalimbali, hivi sasa wanazo taasisi mbalimbali za kudhibiti ujangili.
“Tuna kamati, vyombo, task force (vikosi kazi) vya aina mbalimbali kwenye ardhi, majini na angani ili kuhakikisha kuwa, suala la ujangili wanalidhibiti vizuri kabisa,” amesema.
Pia, amesema wanaendelea kuhakikisha uhifadhi endelevu na mapito ya wanyama ili kuimarisha mifumo ya ikolojia ya uhifadhi.
Aidha, amesema wanaendelea kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika usimamizi wa wanyamapori kupitia Jumuiya za Uhifadhi ya Wanyamapori (WMA).
Dk Chana amesema Serikali imeendelea kutoa mgawo wa fedha kwa halmashauri za wilaya, vijiji na WMA na kutoa rai kwa halmashauri za wilaya na vijiji na kuendelea na kutenga maeneo ya uhifadhi.
Amesema lengo ni kuendeleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ulinzi wa wanyamapori na kuendelea kudhibiti migongano ya wanyamapori wakali na waharibifu, kutoa mafunzo na kununua vitendea kazi mabomu baridi na ndege nyuki.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara hiyo, katika kipindi cha mwaka 2022/23, Serikali ilitoa gawio la Sh10.2 bilioni kwa halmashauri za wilaya na vijiji pamoja na WMA huku mwaka 2023/24, ikitoa Sh13.1 bilioni kwa makundi hayo ya uhifadhi.
Mkurugenzi wa wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Alexander Lobora amesema Serikali imeendelea kuandaa mkakati wa kuokoa aina mbalimbali ya wanyamapori adhimu au walioko hatarini kutoweka.
Amewataja wanyama hao ni faru, duma, sokwe na wengine, pamoja na utekelezaji wa programu ya mauaji ya tembo nchini chini ya Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Wanyama na Mimea Walio Hatarini Kutoweka (CITES) na ufuatiliaji wa biashara ya nyara za Serikali.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Benedict Wakulyamba amesema tangu Serikali iridhie mkataba wa CITES mwaka 2014, wamekuwa wakiadhimisha Siku ya Wanyamapori Duniani.