Serikali yapangua hoja za ACT-Wazalendo

Unguja. Siku chache baada ya ACT- Wazalendo kuitaka Serikali kuvunja mkataba wa uendeshaji wa Bandari ya Malindi kati ya Shirika la Bandari (ZPC) na Kampuni ya Africa Global Logistic (AGL) ya Ufaransa, Serikali imesema haina mpango kwa sababu kampuni hiyo imeonesha ufanisi mkubwa.

Akizungumza leo Jumapili, Machi 2, 2025 na waandishi wa habari, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed amesema taarifa zilizotolewa na chama hicho ni za upotoshaji na hawawezi kusema wavunje mkataba kisa mtu mmoja au kikundi fulani bali wanaangalia maslahi ya wananchi na Taifa.

Hata hivyo, amesema iwapo ikifika hatua ikaona kuna haja haitasita kufanya hivyo na kwamba, hoja zilizotolewa na chama hicho hazina uhalisia bali zinalenga kuleta taharuki kwa wananchi.

Amesema tangu Serikali iingie makubaliano ya kuendesha bandari hiyo mwaka 2023 kuna mafanikio makubwa na ufanisi huku mapato yakiendelea kuongeza kwa asilimia 41 na ufanisi wa kushusha na kupandisha makasha, ukitajwa kuongezeka.

Serikali kupitia ZPC ilikabidhi Kampuni ya AGL chini ya kampuni yake tanzu ya Zanzibar Mult Terminal (ZMT) kuendesha Bandari ya Malindi kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Septemba 18, 2023.

Februari 27, 2025 akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa  ACT- Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa alitaja hoja mbalimbali ikiwamo mapato kushuka, kuingia mifukoni mwa watu, kampuni hiyo kutokuwa na vifaa, kuongezeka kwa tozo, wafanyakazi kushushiwa mishahara na wengine kuachwa kwenye mikataba mipya ya kampuni hiyo.

Hata hivyo leo waziri amesema: “Kwa sasa haiwezekani kuvunja mkataba, kuna viwango viliwekwa (KPI) ambavyo vinaangaliwa tangu tunaingia mkataba huu, kwa hiyo kusema kwamba mtu mmoja hajaridhika, hatuwezi kwenda namna hiyo, tutavunja mkataba iwapo kweli tukiona kuna shida.”

“Serikali ilifikia hatua ya kutafuta mwendeshaji wa bandari kutokana na changamoto zilizojitokeza, ufanisi mdogo wa bandari huku ikisababisha baadhi ya meli kuacha kuja Zanzibar kwa kukosa ukuta kushusha mizigo.”

Dk Khalid amesema zilijitokeza kampuni nne katika uwekezaji huo, lakini kampuni moja ya AGL ndio ilionekana kukidhi viwango si kwasababu tu ya uzoefu wake, lakini ilitoa asilimia 30 kama mrabaha kwa Serikali huku ikibeba gharama zote za uendeshaji na wafanyakazi wote waliokuwa ZPC kuwachukua.

Amesema wakati kampuni hiyo inaanza kazi, muda wa meli kukaa nangani ilikuwa ikitumia siku 20 hadi 40 lakini baada ya kuanza kazi inatumia wastani wa siku nane.

Hata hivyo, kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, amesema ndio muda umeongezeka tena kufikia siku 18 za kukaa nangani sababu kubwa ikitajwa ni kuongeza kwa mahitaji ya bidhaa kulinganana na mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao kwa kipindi hicho mahitaji yanakuwa makubwa.

Kuhusu hoja ya kwamba Serikali ilinunua vifaa vya Sh17 bilioni na ikatumia fedha vibaya ikijua anakuja mwekezaji, Dk Khalid amesema wakati vinanunuliwa vifaa hivyo bado walikuwa hawajaingia mkataba na kampuni hiyo bali zilikuwa jitihada za kupunguza msongamano huku ikiangalia njia mbadala ya kupata suluhisho la kudumu.

“Kuhusu hoja ya kwamba ZMT hawakununua vifaa bali wanatumia walivyokuta, sio kweli kwani miongoni mwa vifaa ambavyo wamenunua ni pamoja na Mobile Krane ambayo ina uwezo mkubwa katika kushusha na kupakia makasha,” amesema Dk Khalid.

Amesema baada ya kampuni hiyo ya kigeni kuanza uendeshaji wake imepunguza msongamano Bandari ya Malindi kwa kujenga bandari kavu eneo la Maruhubi lenye ukubwa wa hekta mbili kwa gharama ya Dola 5 milioni za Marekani huku ikitarajia kuongeza ekari moja.

Kwa sasa kuna jumla ya ekari 11 za kuhifadhi makontena kutoka ekari tano zilizokuwapo awali.

Kuhusu muda wa wateja kupata mizigo yao, Dk Khalid amesema imetokana na mabadiliko ya mifumo lakini wamekubalina na ZMT kuongeza saa za kufanya kazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa mbili usiku badala ya saa 11 iliyokuwapo awali.

Siku za Jumamosi inaanza kufanya kazi saa 2:00 asubuhi hadi saa 11: 00 jioni na siku za Jumapili wamepeleka maombi maalumu kwa kampuni hiyo ili angalau ifanye kazi kwa saa chache kutokana na siku hiyo kuwa ya mapumziko.

Akifafanua hoja ya kuongezeka kwa tozo mbalimbali zilizodaiwa na chama hicho, Dk Khalid amesema hakuna kilichoongezeka isipokuwa mwendeshaji anafuata kitabu cha miongozo cha mwaka 2018, hivyo kuna baadhi ya huduma zilikuwa zimetajwa lakini zilikuwa hazitumiki baada ya mwekezaji huyo, zilianza kutozwa.

“Mfano tozo za kusafirisha makontena kutoka bandarini kwenda bandari kavu hazikuwapo kwa sababu kwanza hakukuwa na bandari kavu, pia tozo za krane zilikuwa kwenye mwongozo lakini zilikuwa hazitozwi,” amesema Dk Khalid.

Kwa upande wa wafanyakazi kupunguziwa mafao yao, Waziri amesema baada ya mwendeshaji huyo kupewa bandari waliokuwa wakilipwa mshahara kati ya Sh600,000 hadi Sh800,000 wameongezewa hadi kufika Sh1 milioni (wanaoendesha mashine) wakati upande wa watendaji bado wapo kwenye mpango wa kubadilisha mishahara hiyo.

Akifafanua zaidi kuhusu mapato ya bandari, Mkurugenzi wa ZPC, Ali Akif amesema wastani wa mapato kwa mwezi yameongezeka kutoka Sh1 bilioni hadi kufikia Sh2 bilioni baada ya kuondoa gharama zote za uendeshaji.

Amesema wakati kampuni hiyo inakabidhiwa bandari hiyo, Serikali ilikuwa inapata Sh1.4 bilioni kwa mwezi na sasa inapata Sh2.6 bilioni kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 41.

“Kwa hiyo kuanzia Septemba 18, 2023 tangu alipokabidhiwa bandari hii mpaka kufikia Januari 2025, Serikali imepata Sh29.3 bilioni kama faida,” amesema