
Dar es Salaam. Serikali imeondoa zuio la biashara na usafirishaji wa mazao ya kilimo kati ya Tanzania na nchi za Malawi na Afrika Kusuni baada ya kudumu kwa siku mbili.
Kupitia Wizara ya Kilimo Aprili 23, 2025 ilitangaza kuzuia mazao kutoka nchi za Afrika Kusini na Malawi kuingia katika mipaka ya Tanzania hadi hapo hatua zitakapochukuliwa kwa nchi hizo kuruhusu mazao yetu kuingia katika masoko yao.
Kufuatia zuio hilo, Serikali za Malawi na Afrika Kusini zimewasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Kilimo za Tanzania ili kuweza kutafuta suluhisho la zuio husika.
Katika taarifa hiyo Waziri Bashe jana Aprili 25, 2025 amesema makubaliano yaliyofikiwa ni kwamba Serikali ya Malawi itatuma ujumbe wake Mei 2, 2025 utakaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje akiambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kilimo ili kukutana na ujumbe wa Tanzania jijini Dodoma chini ya uratibu wa Waziri wetu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kuhusu zuio la Afrika Kusini, majadiliano ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania yanaendelea kwa pamoja na Mamlaka za nchi ya Afrika Kusini zinazohusiana na Afya ya Mimea na Masoko.
“Kwa misingi hiyo, Wizara ya Kilimo inaondoa mazuio yote yaliyowekwa kwa nchi za Malawi na Afrika Kusini kuanzia tarehe 26 Aprili, 2025 tukiamini kuwa majadiliano yanayoendelea yataleta suluhisho,” imeeleza taarifa hiyo.
Bashe amesema Serikali inawahakikishia wakulima na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kuwa, uhuru wa biashara ya mazao ya kilimo kulingana na matakwa ya afya ya mimea, rasilimali za nchi zilizopo na mahusiano mapana ya kidiplomasia kwa faida ya wote.