Dar es Salaam. Serikali yaomba muda kukamilisha upelelezi kesi ya msanii wa fani ya uigizaji, Joyce Mbaga (32) maarufu Nicole Berry na mwenzake, Rehema Mahanyu (31), wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Msanii huyo na mwenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni, Jumatatu Machi 10, 2025, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kutokana na kupokea amana (fedha) kutoka kwa umma bila kibali cha Benki Kuu (BoT).

Kesi hiyo ilipotajwa leo, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Rhoda Kamungu ameieleza Mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika.
“Mheshimiwa Hakimu kesi hii imepangwa leo kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika. Hivyo tunaiomba Mahakama yako itupangie tarehe nyingine ya kutajwa,” amesema Wakili Rhoda.
Taarifa hiyo ya upelelezi kutokukamilika na maombi ya kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa, kwao hiyo inamaanisha Serikali kupewa muda wa kuendelea na upelelezi.
Mawakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya na Wilson Magoti, wamelieleza Mahakama kuwa hawana pingamizi kwa taarifa hiyo ya Serikali kuhusu hali ya upelelezi na maombi ya ahirisho na kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Rugemalira amekubaliana na taarifa na maombi hayo ya Serikali na ameahirisha kesi hiyo mpaka Aprili 14, 2025, itakapotajwa kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika kabla ya kuendelea na hatua nyingine.
“Kesi hii itatajwa tena Aprili 14, 2025 na washtakiwa mtaendelea kuwa nje kwa dhamana,” amesema Hakimu Rugemalira.
Katika kesi hiyo, Nicole na mwenzake wanakabiliwa na mashitaka matatu, wanayodaiwa kuyatenda kati ya Julai 2024 na Machi 2025 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Shitaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu kwa lengo la kujipatia fedha, la pili ni kupokea fedha kutoka kwa umma bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na shitaka la tatu ni kuendesha mfumo wa malipo bila kuwa na leseni ya malipo kutoka BoT.
Katika shtaka la kwanza, Wakili Rhoda alidai kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo kwa lengo la kujipatia faida kwa kupokea amana au miamala kutoka kwa jamii bila kupata leseni.
Katika shitaka la pili, alidai kuwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025, wakiwa eneo lisilofahamika ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, walipokea amana ya Sh185,515,000 (Sh185.51 milioni) kutoka kwa jamii bila kuwa na leseni.
Katika shitaka la tatu, Wakili Rhoda alidai kuwa washtakiwa waliendesha mfumo wa malipo bila kuwa na leseni ya malipo inayotolewa na BoT.