Serikali yamalizia mchakato kuifanya NEMC kuwa mamlaka

Dar es Salaam. Serikali imesema inaendelea na mchakato wa kufanya mabadiliko ya kisheria ili kulibadilisha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwa mamlaka kamili itakayokuwa na nguvu zaidi katika kushughulikia changamoto mbalimbali za mazingira nchini

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi, Mei 3, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, wakati wa kampeni ya usafi wa fukwe iliyofanyika katika ufukwe wa Mbali, uliopo Mbezi Beach B.

Kampeni hiyo ya usafi wa mazingira, ambayo imefadhiliwa na Ubalozi wa Ufalme wa Saudi Arabia na kuratibiwa na Mtandao wa Haki za Binadamu Afrika (AHRN), imekusudia kutunza mazingira ya fukwe za bahari za jijini Dar es Salaam.

Masauni amesema mabadiliko hayo ya kisheria yanakusudia kuimarisha uwezo wa NEMC pamoja na mamlaka yake ya utekelezaji wa sheria.

“Natambua kuna hoja ya changamoto ya kisheria, ambayo tunaenda nayo vizuri, ya mabadiliko ya sheria ya kuifanya NEMC iwe Mamlaka. Kuna hoja kwamba tunadhani NEMC ikipata meno zaidi inaweza kusimamia kwa nguvu zaidi changamoto mbalimbali za mazingira,” amesema Masauni.

Masauni ametumia nafasi hiyo kuwahimiza Watanzania kuwajibika katika kulinda mazingira hata kabla ya sheria kuboreshwa, akisisitiza kuwa NEMC inapaswa kusimamia sheria kwa haki bila woga au upendeleo.

“NEMC ihakikishe inasimamia sheria bila kumwonea haya mtu. Sheria hizi zilizopo tutazirekebisha ili kuzipa meno zaidi. Tunadhani hatua zitakuwa kali zaidi,” amesema

Pia amewataka wananchi kuendeleza nidhamu ya mazingira, hususan katika maeneo ya fukwe za bahari.

“Jambo la usimamizi wa mazingira linaanzia katika ngazi ya familia, linakuja kwa jamii, na Serikali yenyewe inatakiwa ichukue jukumu lake la kusimamia,” amesema.

Katika kushughulikia hilo, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za taka, ikiwamo kutunga Sera ya Taifa ya Mazingira (2021), Mpango Mkakati wa Taifa wa Mazingira (2022–2032), Mwongozo wa Uwekezaji katika Usimamizi wa Taka, na Mwongozo wa Taifa wa Usimamizi wa Taka Ngumu kupitia dhana ya Punguza, Tumia Tena na Tumia Upya (3Rs).

Kwa upande wake, Balozi wa Ufalme wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Yahya Okeish, amesema kampeni hiyo inaonesha dhamira ya nchi yake katika kulinda mazingira ya kimataifa na kushirikiana na mataifa rafiki duniani.

Amesema kampeni hiyo ni sehemu ya programu ya kitaifa ya kujitolea ya Saudi Arabia inayolenga kuendeleza maadili ya pamoja kupitia sera zake za nje.

Balozi Okeish amewahimiza Watanzania kuendelea kutunza fukwe za Mbezi na maeneo mengine ya fukwe kwa manufaa ya jamii na vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa AHRN, Olivier Muhizi, amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kunakuwepo na kituo cha kuchakata taka ambacho kitakuwa kinakusanya na kuchambua taka zote.

“Tutakuwa tunakusanya takataka zote, tunachagua plastiki tunaziweka pembeni, tunachagua zile ambazo zinaweza kutumika kutengeneza vifaa vingine mbalimbali, na zile ambazo zinaweza kuoza tunaziweka sehemu sahihi ili ziweze kutumika kwa kutengenezwa zaidi kama mbolea, zinaweza zikatumika kutengeneza mkaa,” amesema Muhizi.

Amependekeza kampeni ya usafi wa fukwe ifanyike kila mwezi ili kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa jiji safi zaidi barani Afrika.

“Lengo letu ni Dar es Salaam iwe inasifiwa kuwa mji wa kwanza msafi Afrika nzima,” amesema.

Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Jenerali Patrick Nyamvumba, aliyeshiriki pia katika tukio hilo, amesisitiza kuwa ni jukumu la bara la Afrika kuchukua hatua kubwa zaidi kurejesha na kulinda rasilimali za asili zinazopotea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *