
Unguja. Ili kukuza uchumi wa kidijitali, Serikali ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti kwa kusaini makubaliano (MoU) ya ujenzi wa kituo cha kukuza ubunifu na Ujasiriamali wa Tehama Zanzibar utakaogharimu zaidi ya Sh2 bilioni.
Hafla ya utiaji saini imefanyika mwishoni mwa wiki kati ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa uchumi wa kidijitali uliozinduliwa Juni 2024.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Nkundwe Mwasaga amesema ujenzi wa kituo hicho unaotarajiwa kuanza hivi karibuni ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mazingira ya ubunifu wa Tehama nchini.
Aidha kuhakikisha wabunifu wa teknolojia wanapata nafasi ya kuendeleza mawazo yao na kuyageuza biashara zenye tija kwa Taifa.
“Tunaelekea kwenye uchumi unaotegemea maarifa, na hivyo hatuwezi kupuuza umuhimu wa kuwekeza kwenye miundombinu ya ubunifu wa Tehama. Vituo hivi vitakuwa na vifaa na rasilimali zinazowawezesha wabunifu wetu, wajasiriamali na vijana wanaoanzisha kampuni za teknolojia kupata nafasi ya kuendeleza miradi yao kwa ufanisi,” amesema.
Ameongeza kituo cha Zanzibar ni sehemu ya mtandao wa vituo 10 vya kukuza ubunifu wa Tehama vinavyojengwa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, ikiwemo Mwanza, Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Tanga na Lindi.
Lengo la vituo hivi ni kusaidia kuharakisha maendeleo ya sekta hiyo kwa kuwapatia vijana mazingira mazuri ya kujifunza, kubuni, na kuanzisha biashara zinazotumia Tehama.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amepongeza juhudi hizo na kusisitiza kituo hicho kitakuwa muhimili muhimu wa kukuza sekta ya Tehama Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
“Nchi yetu inahitaji mifumo thabiti ya ubunifu wa Tehama ili kuhakikisha vijana wetu wanakuwa sehemu ya mapinduzi ya kidijitali yanayoendelea duniani. Kituo hiki siyo tu kitawawezesha vijana kubuni suluhisho za kidijitali, bali pia kitawasaidia kupata mafunzo, ushauri wa kitaalamu, na hata kufungua fursa za kimataifa,” amesema Dk Khalid.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Habiba Hassan Omar amesema kuwa Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha Tehama inakuwa sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu na wajasiriamali wa teknolojia.
Miongoni mwa malengo ya kituo hicho cha ubunifu ni pamoja na kuimarisha ubunifu na kusaidia wabunifu wa teknolojia kuendeleza miradi yao, kujenga mnyororo wa thamani wa ubunifu wa Tehama, kutoa fursa za ajira na kuzalisha kampuni changa za Tehama, kuwezesha ushirikiano wa kimataifa kwa wabunifu.