Serikali yajivunia mageuzi yaliyofanywa na Rais Samia sekta ya afya

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel amesema wanajivunia maboresho makubwa yaliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afya kwa miaka minne hatua iliyowezesha

Akizungumza Aprili 4,2025 kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Afya ambayo yanaendelea kufanyika nchini Dk. Mollel amesema Rais Samia amefanya mapinduzi makubwa kwenye miundombinu ya afya, teknolojia tiba, kuongeza ujuzi wa wataalam.

Ametolea mfano kuwa wakati Rais Dk. Samia anaipokea nchi ni hospitali mbili tu za mikoa zilikuwa na teknolojia ya CT Scan hatua iliyosababisha wananchi wa Nyanda za Juu Kusini waende Mbeya kupata huduma lakini kwa sasa huduma hiyo inapatikana katika kila mkoa.

“Mtu anatoka Kigoma anakwenda Mbeya kufuata huduma ya CT Scan na wengine walikuwa wanatoka mikoa mingine wanakuja Dar es Salaam lakini leo CT Scan imefika kila mkoa na watu wote wanapata huduma, kwa kipindi kifupi cha urais wa Dk. Samia maana yake ameweza kuokoa asilimia 78 ya watu waliokuwa wafe kwa kansa,” amesema Dk. Mollel.

Kuhusu teknolojia ya tiba ya saratani amesema awali walikuwa wanakwenda kuchukua mionzi tiba Afrika Kusini na Uturuki lakini kwa sasa kuna kiwanda cha kuzalisha mionzi tiba nchini sambamba na mashine yenye uwezo wa kugundua saratani inayoweza kutokea miaka miwili hadi 10 ijayo.

“Kwa hiyo unaweza kwenda kwenye taasisi yetu ya Ocean Road wakagundua kansa ambayo ingeweza kutokea baadaye ukaanza kutibiwa. Unafanyiwa operesheni chini ya sakafu ya ubongo kupitia kwenye pua, unaweza kupata shida nyingine kwenye ubongo ilihitaji ufunguliwe mfano kwenye mishipa ya damu ilikuwa lazima ufunguliwe kichwa lakini leo kwa teknolojia unaweza ukapitia mshipa mkubwa ulioko mguuni ukatibiwa bila kupasua kichwa.

“Tunawaalika Watanzania waje waone miujiza aliyofanya Dk. Samia kwenye sekta ya afya, kwa miaka minne amefanya mapinduzi makubwa kwenye miundombinu, teknolojia tiba, kuongeza ujuzi wa wataalam na anatamani baadhi ya teknolojia zianze kuzalishwa hapa nchini.

“Tunajadili na wataalam kwamba kwanini Tanzania tusianze kuenzi na kutengeneza watu wanaoweza kuja na ‘solution’ ya matatizo na si kwa kunakili kwa watu wengine duniani,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk. Mollel mageuzi katika sekta ya afya yamesababisha mataifa mbalimbali kuja Tanzania kutibiwa hasa nchi zilizotuzunguka ambapo ilikuwa waende India, Ulaya, Marekani lakini kwa sasa wanatumia gharama ndogo kuja nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *