Serikali yaja na mwarobaini wauzaji mbegu feki

Dodoma. Serikali ya Tanzania imetaja mikakati ya kukabiliana na mbegu feki nchini, ikiwemo kusajili upya wauzaji wa vijijini na wa mikoani pamoja na kuubadili mfumo wa usambazaji.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Mei 15, 2025, na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Thea Ntara.

Katika swali la nyongeza, Ntara alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha mbegu zinazouzwa dukani zote zina ubora na zinapatikana kwa bei nafuu ili wanawake waweze kuzinunua kwa uhakika.

Akijibu swali hilo, Bashe amesema suala la ubora linaendelea kufanyiwa kazi kwa kuiwezesha Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), na kwamba msimu ujao wa kilimo, wakulima wataona lebo mpya itakayowekwa kwenye mifuko yote ya mbegu sokoni.

“Ili kutatua tatizo la mbegu feki, Serikali imeamua kusajili upya wauzaji wa vijijini na wa mikoani, na kuubadili mfumo wa usambazaji. Kuanzia sasa, wasambazaji wote wataingizwa kwenye kanzidata maalumu,” amesema Bashe.

Kuhusu suala la kupunguza gharama za mbegu, Bashe amesema Serikali imeweka ruzuku katika mbegu, na walianza na ngano, alizeti, na sasa wameongeza zao la mahindi.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inawapunguzia wakulima gharama za mbegu.

Ameongeza kuwa Serikali imeanza kuihusisha sekta binafsi kwa kutumia mashamba ya Serikali ambayo yalikuwa hayatumiki na yamegeuka mapori, kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu ili zipatikane kwa wingi na bei nafuu.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mwanaisha Ulenge, amehoji mkakati wa kuwaandaa wanawake wakulima wa mbogamboga wa Mkoa wa Tanga kwenye mpango wa Tanga kuwa Hub ya kilimo cha mbogamboga.

Akijibu swali hilo, Bashe amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekiwezesha Kituo cha Utafiti cha Mlingano (TARI Mlingano) kuwa kituo mahiri katika uzalishaji wa mazao ya viungo, ikiwemo karafuu.

Pia, amesema wizara inaendelea kutoa mafunzo ya kanuni na teknolojia bora za kilimo cha mbogamboga, na kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo Taha kujenga vituo na miundombinu ya kuhifadhi mazao ya mbogamboga, ikiwemo vyumba vya ubaridi.

Ameongeza kuwa wizara inaendelea kutoa mafunzo ya ukusanyaji, ufungashaji na uhifadhi wa mazao kabla ya kusafirishwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Katika swali la nyongeza, Mwanaisha amesema kwa kuwa Serikali imechagua Tanga kuwa miongoni mwa kanda za kuzalisha mazao ya matunda na mbogamboga, luhoji haioni haja ya kutengeneza vifungashio vya kulinda mlaji na kuongeza thamani ya mazao ya wanawake wa Mkoa wa Tanga?

“Kwa kuwa sasa magari ya kuchimba visima yameingia nchini, je, Serikali haioni haja ya kutoa kipaumbele kwa Mkoa wa Tanga kuchimbiwa visima vya umwagiliaji, kwa sababu mazao ya mboga yanakua kwa haraka ili wapate tija mapema?” amehoji Mwanaisha.

Akijibu swali hilo, Bashe amesema mpango wa Serikali ni kutengeneza kanda za uzalishaji wa mazao ya matunda na mbogamboga, na Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa itakayokuwa kwenye kanda hizo.

“Wataalamu wa wizara wameshaanza kufanya tathmini mkoani humo kwa mazao yote; viungo, matunda na mbogamboga, ili kuanzisha mfumo wa ukusanyaji wa mazao, namna ya kuyauza na kuyafungasha,” amesema Bashe.

Amesema mkakati huo unaendelea kupitia upembuzi yakinifu katika maeneo yaliyoteuliwa kwa ajili ya uzalishaji wa mbogamboga, matunda na viungo.

“Niwatoe hofu na niwaambie wananchi wa Tanga kwamba hili jambo Serikali inalifanyia kazi, na hivi karibuni tutatangaza lini utekelezaji utaanza,” amesema.

Kuhusu uchimbaji wa visima vya umwagiliaji, Bashe amewahakikishia wabunge kuwa mikoa yote itapewa kipaumbele, lakini kipaumbele kikubwa kitapewa maeneo ambayo tathmini imeshafanyika.

“Mpaka sasa tathmini imeshafanyika kwa halmashauri 75 ambazo zitaanza kufanyiwa utaratibu wa kuchimbiwa visima, hivi karibuni Serikali itatangaza utaratibu rasmi kupitia mwongozo,” amesema.

Amesema kutakuwa na skimu ambayo baadhi ya wakulima watachimbiwa visima bure kwa asilimia 100, na kutakuwa na wakulima ambao watachangia gharama kidogo.

“Mfumo wa uchimbaji hautakuwa kila mkoa kupelekewa gari. Serikali imenunua magari 23 ambayo kufikia Juni 15 yatakuwa yamefika yote, ndipo tutatangaza ni mkoa gani tunaanza kuchimba,” amesema.

Amewaomba wabunge kusubiri tangazo la umma litakalotolewa kwa kila mkoa, ili kufahamu ni lini magari hayo yatakwenda katika mkoa husika.

Mbunge wa Ilemela (CCM), Dk Angelina Mabula, amesema Manispaa ya Ilemela ina wakulima wachache wa mboga kutokana na eneo dogo. Akauliza iwapo Serikali haioni haja ya kuwaanzishia vitalu nyumba ili wazalishe kwa tija.

Akijibu swali hilo, Bashe amemhakikishia mbunge huyo na wakulima wa Ilemela kuwa Serikali inalifanyia kazi suala hilo.

“Baada ya bajeti ya mwaka huu, wakulima wa maeneo hayo na Ziwa Victoria yote wataona tumeweka mpango kwa ajili yao,” amesema Bashe.

Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe, amesema wakulima wa nyanya ni wengi wilayani Hai na bei imeshuka kutokana na wingi wa uzalishaji. Akauliza Serikali ina mpango gani wa kujenga kiwanda cha kuchakata zao hilo.

Akijibu swali hilo, Bashe amesema wamelipokea suala hilo na wanaangalia namna ya kuongeza thamani kwenye zao hilo.

Amesema katika bajeti ijayo watakuwa na mpango maalumu wa kuongeza thamani ya mazao yote ili kuongeza kipato cha wakulima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *