Serikali yaiweka njiapanda kesi Mpina na Spika

Dar es Salaam. Kesi ya Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhwaga Mpina aliyoifungua dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na wenzake wawili iko njia panda baada ya Serikali kupingamizi la awali ikipinga Mahakama kuisikiliza.

Katika kesi hiyo ya Kikatiba, Mpina anapinga uamuzi wa Spika wa Bunge na utaratibu uliotumika kumpata adhabu ya kumsimamisha kuhudhuria vikao 15 vya Bunge hilo, kwa tuhuma za kusema uwongo dhidi ya Waziri wa Kilimo.

Awali, Mpina aliibua hoja ya vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi akimtuhumu Waziri wa Kilimo kukiuka sheria katika utoaji wa vibali hivyo na Spika Tulia Akson akamtaka awasilishe ushahidi uliopelekwa katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka kuupitia.

Juni 24, 2024, Kamati hiyo iliwasilisha bungeni ripoti yake pamoja na mambo mengine ikisema tuhuma za Mpina dhidi ya Waziri wa Kilimo zilikuwa za uwongo.

Kutokana na ripoti hiyo, Bunge chini ya Spika Tulia lilipitisha azimio la adhabu ya kumsimamisha Mpina kuhudhuria vikao 15.

Hata hivyo, Mpina hakukubaliana na uamuzi huo, ndipo akafungula kesi ya Kikatiba dhidi ya Spika wa Bunge, Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hiyo, anapinga uamuzi wa kumsimamisha akidai hakupewa haki ya kusikilizwa kabla ya kupitishwa uamuzi huo na kwamba taratibu zilikiukwa huku akibainisha kasoro mbalimbali.

Hata hivyo, Serikali imeibua pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo ikiiomba Mahakama iitupilie mbali bila kuisikiliza huku ikibainisha sababu tatu za pingamizi hilo.

Pingamizi hilo limesikilizwa leo Jumanne, Septemba 24, 2024, na Jaji Awamu Mbagwa;  Serikali ikifafanua hoja zake za kupinga shauri hilo huku mawakili wa Mpina nao wakazipinga hoja hizo vikali.

Katika sababu ya kwanza ya pingamizi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Edwin Webiro amesema Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza shauri hilo.

Wakili Webiro amefafanua hoja hiyo huku akirejea kesi mbalimbali zilizoamuriwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kuwa Mahakama haina mamlaka ya kuhoji uhalali wa uamuzi au mwenendo wa Bunge kwa sababu za kasoro za kiutaratibu.

Badala yake amesema Mahakama inaweza kuhoji mambo yaliyofanywa na Bunge nje ya mamlaka yake iliyopewa Kikatiba.

Amesema kwa mambo yaliyofanywa na Bunge yaliyo katika mamlaka yake Mahakama haiwezi kuyahoji hata kama utaratibu utakuwa umekiukwa na kwamba huo ndio msingi wa mgawanyo wa madaraka ya mihimili hiyo mitatu ya dola chini ya Ibara ya 4 ya Katiba.

Wakili Webiro amesema msimamo huo ulisisitizwa na Mahakama hiyo katika kesi ya Agustine Lyatonga Mrema dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania, Shauri la maombi mchanganyiko namba 36 la mwaka 1998.

Wakili Webiro amesema katika kesi hiyo ya Mrema, Mahakama ilijiuliza swali iwapo Bunge lilikuwa na mamlaka ya kumsimamisha mbunge.

Wakili Webieo amesema Mahakama katika kesi hiyo ilidhihirisha kuwa, Bunge lina mamlaka hayo na kwamba katika uamuzi wake ilisema, kwa kuwa Kanuni za Kudumu za Bunge zinaruhusu mbunge kusimamishwa kwa sababu au mambo yanayotokea bungeni, siyo kinyume cha Katiba (hatua/ uamuzi huo).

“Mheshimiwa Jaji, mwombaji anahoji mwenendo wa Bunge na matokeo yake kwa sababu ya kasoro za utaratibu, alidai ripoti ya Kamati ya Haki Maadili na Madaraka ya Bunge iliyomtia hatiani ilikiuka utaratibu na Kanuni za Kudumu za Wabunge kwa kupendekeza adhabu,” amesema Wakili Webiro.

Wakili Webiro ametaja mambo mengine ambayo Mpina anayalalamikia kuwa ni kasoro za kiutaratibu katika kusimamishwa kwake na Spika kutoa maoni kuhusiana na adhabu kabla ya ripoti ya Kamati ya Haki na Maadili, jambo analodai kuwa na hivyo kuathiri uhuru wa Kamati hiyo.

Pia, anadai Kamati iliwasilisha taarifa yake bila kuwekwa kwenye ratiba ya shughuli za Bunge za simu hiyo na kwamba, Spika alikiuka kwa kuwaalika wabunge kupendekeza adhabu ya kusimamishwa kwa vikao 15 bila kupitisha maazimio kwa mujibu kanuni ya 68(7) ya Kanuni za Bunge.

Badala yake anadai ajenda ya ripoti ya kamati hiyo iliwasilishwa kupitia mlango wa nyuma.

Mwisho Mpina anadai mwenendo wa shughuli za Bunge kuhusiana na ripoti ya Kamati, ulikiuka kanuni ya kawaida inayoongoza shughuli za Bunge ambayo ni 34(4) (5) za Kanuni za Kudumu za Bunge.

Kutokana na madai hayo Wakili Webiro amedai Mpina anapinga kasoro za mamlaka ya Bunge au kutokuzingatiwa kwa kanuni na utaratibu unaosimamia shughuli za Bunge na anadai Bunge lilitenda nje ya mamlaka yake au kwamba lilitekeleza mamlaka ambayo halina.

Hivyo amedai kwa kuwa wameonesha Bunge lina mamlaka kumsimamisha mwombaji chini ya Kanuni 84 ya Kanuni za Bunge na kwa kuwa mwombaji anapinga kasoro au kutokuzingatiwa kanuni za utaratibu basi Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Wakili Webiro amesema katika kesi ya Mrema na Spika, Mahakama hiyo iliamua katika mazingira hayo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na akasisitiza haina mamlaka ya kusikiliza hiyo ya Mpina.

Amedai Mpina kwa kufungua kesi hiyo kwa kupinga maamuzi ya Bunge ya kumsimamisha yaliyofanywa bungeni, amekiuka Ibara ya 101 ya Katiba.

Katika kutia uzito hoja yake Wakili Webiro pia ameirejesha Mahakama katika uamuzi wa kesi moja iliyoamuriwa na Mahakama ya India kuhusiana na uamuzi wa Bunge kumsimamisha mbunge.

“Kwa kuzingatia hoja tulizoziwasilisha hapo, ni hoja yetu kwamba kwa kuwa Bunge lina mamlaka ya kumsimamisha mwombaji, Mahakama hii inazuiwa kushughulikia shauri hili kutokana na kesi rejea hizo tulizoziwasilisha,” amesema Wakili Webiro.

Katika sababu ya pili ya pingamizi, Wakili Webiro amedai mwombaji alikuwa na njia mbadala ambayo angeweza kuitumia kabla ya kuja mahakamani.

Amesema kwa kuwa Mpina anahoji uamuzi wa Spika, alipaswa kutumia Kanuni za Bunge hasa Kanuni ya 5 (4) inayoeleza kama mbunge hakubaliani na uamuzi wa Spika anatakiwa kuwasilisha malalamiko yake kwa Spika kwa maandishi kupitia kwa Katibu wa Bunge akiele sababu za kutokuridhika.

Kwa hiyo, Wakili Webiro amesema kuwa kwa kuwa Mpina anapinga uhalali wa uamuzi wa Spika alipaswa kutumia nafuu hiyo ya Kanuni ya 5 (4) ya Kanuni za Kudumu za Bunge kabla ya kufungua shauri hilo.

Wakili Webiro huku akirejea uamuzi wa kesi mbalimbali zilizoamuriwa na Mahakama, amesema kuwa ni msimamo wa Mahakama kwamba pale ambapo mwombaji anakuwa na nafuu mbadala anapaswa kutumia njia hizo kwanza kabla ya kufungua shauri la Kikatiba.

Pia, amesema kuwa kwa kuwa Mpina analalamikia uamuzi wa Spika na Kanuni kuwa zimekiukwa basi alipaswa kufungua kwanza shauri la Mapitio ya Mahakama kabla ya kufungua kesi ya Kikatiba.

Katika sababu ya tatu, wakili Webiro amedai kwa kuisoma hati ya madai yote hakuna sababu ya madai dhidi ya mdaiwa wa pili, Waziri wa Kilimo na kwamba hakuna nafuu zozote anazoziomba dhidi yake.

Hivyo, ameiomba Mahakama madai dhidi ya Waziri wa Kilimo yatupiliwe mbali na madai yake shauri liendelee dhidi ya Spika na AG tu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Obadia Kameya amesema kuwa chini ya Ibara ya 89 (1) ya Katiba ya Nchi, Bunge linaweza kutunga Kanuni za Kudumu kwa ajili ya kuweka utaratibu wa shughuli zake.

Hivyo, amesema kwa mujibu wa Kanuni ya 2(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, kama jambo halijawekewa utaratibu, Spika ataamua kwa kufuatia Katiba Kanuni nyingine na mila na desturi za mabunge mengine na uamuzi huo utawekwa kwenye kitabu cha Bunge.

Kwa kanuni hiyo Wakili Kameya amesema kuwa, Bunge linapoendesha shughuli zake halipaswi kuingiliwa na mihimili au chombo chochote na kwamba kwa msingi huo Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Kesi hiyo imeahirishwa kwa muda kabla ya mawakili wa Mpina kuanza kujibu hoja hizo za pingamizi la Serikali.