Serikali yafungua milango ya fursa kwa Diaspora

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewakaribisha Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kuja kuwekeza nchini katika sekta za kiuchumi na kijamii, huku akiwataka watangaze sifa njema ya Tanzania badala ya kuisema vibaya.

Rais Samia amebainisha hayo leo Jumatatu, Mei 19, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya uzinduzi wa toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ya mwaka 2024.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete,  Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmoud Thabit Kombo, Katibu Mkuu Kiongozi, Moses Kusikuka na Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rabia Ahmed.

Wengine waliohudhuria ni watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje, mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania, mabalozi wastaafu, wawakilishi wa sekta binafsi na viongozi wa dini.

Sera hiyo iliyozinduliwa leo na Rais Samia ni utekelezaji wa maelekezo yake aliyoyatoa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na inachukua nafasi ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001, ikiwa imeboreshwa kuendana na mabadiliko yaliyotokea katika kipindi cha miaka 24.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Samia amesema Serikali imewatambua diaspora kama wabia wa maendeleo, hivyo amewakaribisha kuja kuwekeza nchini katika sekta za kiuchumi na kijamii ili kuiletea nchi maendeleo.

“Kwa kuwa sasa Serikali imewatambua kama wabia muhimu wa maendeleo, karibuni nyumbani kwa uwekezaji katika sekta za kiuchumi na kijamii.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali kwenye hafla ya uzinduzi wa Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam leo Mei 19, 2025.

“…na ni wajibu wenu kuitangaza sifa njema ya Tanzania katika nchi mnazoishi badala ya kuisema vibaya nchi yenu,” amesema Rais Samia wakati akihutubia hadhira iliyohudhuria hafla hiyo.

Rais Samia ameeleza hayo wakati diaspora wa Tanzania wakitajwa kutuma fedha kidogo nchini ukilinganisha na mataifa mengine kama Kenya na Nigeria ambako wanatuma fedha nyingi.

Pia, Watanzania waishio nje ya nchi wamekuwa wakipaza sauti zao kuhusu uraia pacha, jambo ambalo halijafanikiwa. Hata hivyo, Serikali limeanzisha mpango wa kuwapa hadhi maalumu ili kuwatambua na kuwawezesha kufanya uwekezaji ikiwemo kumiliki ardhi.

Akemea wanaharakati

Rais Samia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje kutotoa nafasi kwa wanaharakati kutoka mataifa mengine wanaokuja kuingilia mambo ya ndani ya nchi na kuchochea vurugu.

“Tumeanza kuona mtiririko wa wanaharakati ndani ya kanda yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku. Sasa kama kwao wamedhibitiwa, wasije kutuharibia huku.

“Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika, watu wanaishi kwa amani na usalama ni hapa kwetu,” amesisitiza Rais Samia.

Ameongeza: “Niwaombe sana vyombo vya ulinzi na usalama na Wizara ya Mambo ya Nje, kutotoa nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kufanya vurugu hapa. Hapana.”

Rais Samia ameeleza hayo wakati mwanasiasa wa Kenya, Martha Kalua na Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya, Willy Mutunga wakidaiwa kuzuiliwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) na kisha kurudishwa kwao.

Rais wa Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali kabla ya kuzindua Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam leo Mei 19, 2025.

Wakenya hao walikuja nchini kusikiliza kesi ya uhaini na kuchapisha taarifa za uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu. Kesi hiyo iliyosikilizwa leo imeahirishwa hadi Juni 2, 2025

“Nimeiona clip kadhaa za kunisema, kwamba niko bias, ninachofanya ni kulinda nchi yangu. Kwa hiyo hatutatoa nafasi kwa kiumbe yoyote, awe wa ndani au nje ya nchi,” amesisitiza Rais Samia.

Kuhusu sera mpya

Akizungumza kuhusu toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje, Rais Samia amesema ilikuwa ni muhimu kufanya mabadiliko ya sera hiyo kwa sababu kuna mabadiliko mengi yametokea ndani ya miaka 24 ambayo yamebadilisha uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine.

Amesema katika kipindi hicho teknolojia imekua na kuja na changamoto nyingi ambazo lazima wazitazame. Amesema mabadiliko yataendelea kutoka, hivyo ni muhimu kuwa na sera za kujihami kwa kila moja kujilinda.

Mkuu huyo wa nchi amebainisha kwamba katika zama hizi, mataifa makubwa yamekuwa yakipigana vikumbo kupigania nishati za kimkakati ambazo zinapatikana zaidi katika nchi za ulimwengu wa tatu.

“Hilo limebadilisha hali ya kisiasa duniani. Nasi kama sehemu ya Dunia, lazima tutupie macho katika eneo hilo na kurekebisha sera zetu,” amesema Rais Samia.

Katika sera mpya, amesema imezingatia kutumia vema fursa ya kijiografia, kuongeza ushirikiano na sekta binafsi, kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili, kuimarisha uhusiano na mataifa mengine. Ameongeza kuwa sera hiyo pia imezingatia ushirikiano wa kimataifa na Zanzibar.

Mwinyi atoa rai

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametoa rai kwa Wizara ya Mambo ya Nje kuhakikisha kwamba Zanzibar nayo inanufaika na sera hiyo kupitia ushirikiano na mataifa mengine

Pia, ameitaka wizara hiyo kuzishawishi nchi nyingine kuanzisha balozi ndogo au konseli kuu huko Zanzibar ambapo hadi sasa nchi kama China, India na Falme za Kiarabu zimefungua balozi ndogo visiwani humo.

“Nimefurahishwa na namna sera hii ilivyojumuisha maslahi ya Zanzibar. Natoa shukrani za dhati kwa jinsi tulivyoshirikishwa katika uandaaji wa sera hii kwa maslahi yetu sote,” amesema Dk Mwinyi.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmoud Thabit Kombo amesema tangu mwaka 2021 Rais Samia alipoingia madarakani, Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani na kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Amesema sera hiyo ni nyenzo ya kimkakati ya Tanzania kushirikiana na mataifa mengine. Amesema walishirikisha wadau mbalimbali nchi nzima na kupata maoni yao.

“Mapitio ya sera yalianza mwaka 2021 kufuatia maelekezo ya Rais Samia. Tulifanya tathmini kuona kama inahitaji marekebisho. Tanzania imepiga hatua kubwa kiuchumi ambapo mwaka 2020 iliingia kwenye kundi la nchi zenye uchumi wa kati,” amesema.

Waziri huyo amewasilisha mambo maalumu kwa Rais Samia ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo mahsusi kuhusu diplomasia ya uchumi na kuwa na maofisa maalumu wa diplomasia ya uchumi ili kusaidia utekelezaji wa sera hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *