Serikali yaanza operesheni kutokomeza ombaomba mitaani Zanzibar

Serikali yaanza operesheni kutokomeza ombaomba mitaani Zanzibar

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ombaomba mitaani au kuwatumikisha watu wenye ulemavu kwa ajili ya kujinufaisha.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, amesema kuwa Serikali, kupitia uongozi wa Wilaya ya Mjini na wilaya nyingine, inaendelea na operesheni maalumu ya kuwakamata wote wanaojihusisha na shughuli za ombaomba mitaani.

Aliitoa kauli hiyo katika Baraza la Wawakilishi leo, Mei 21, 2025, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, Ameir Abdulla Ameir, ambaye alitaka kufahamu msimamo wa Serikali kuhusu suala hilo ambalo, kwa sasa, linaonekana kuchukua mwelekeo mpya.

Katika maelezo yake, Mwakilishi huyo alieleza kuwa baadhi ya ombaomba katika Manispaa ya Mjini si watu wenye ulemavu, bali wanatumia mbinu hiyo kama njia ya kujipatia kipato kwa udanganyifu.

Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman amesema kuwa ingawa Serikali imekuwa ikitoa kauli kuhusu suala hilo mara kwa mara, bado tatizo hilo linaendelea.

Ameitaka Serikali ieleze wazi ni lini hatua madhubuti zitachukuliwa kulikomesha, akisisitiza kuwa uombaji mitaani si sehemu ya utamaduni wa Mzanzibari.

Akijibu hoja hizo, Waziri Masoud ameeleza kuwa operesheni maalumu tayari zimeanza na kati ya Januari na Machi mwaka huu, Serikali ilifanikiwa kuwakamata watu watatu wanaodaiwa kuwatumia watu wenye ulemavu kwa maslahi yao binafsi.

“Mtakuwa mashahidi kwamba Serikali inaendelea na operesheni hizi. Baadhi ya watu tayari wamekamatwa, na kazi hii inaendelea. Hivyo, tunaamini tutalikomesha tatizo hili,” amesema Waziri.

Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetunga Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 8 ya mwaka 2022, ambayo inalenga kumlinda na kumtetea mtu mwenye ulemavu, kama inavyoelezwa katika vifungu vya 30, 31(1), na 31(2) vya sheria hiyo.

“Sheria hii, pamoja na mambo mengine, inakataza vikali kuwatumikisha watu wenye ulemavu kinyume na haki zao za msingi za kibinadamu,” amesema.

Amesisitiza kuwa suala la uombaji mitaani ni kinyume cha sheria na halilingani na utamaduni wa nchi, hivyo Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kulikomesha.

“Serikali inaendelea na jitihada za mara kwa mara kupitia operesheni maalumu za kuwaondoa ombaomba katika maeneo mbalimbali, hususan maeneo ya Mjini,” amesema.

Ameeleza pia kuwa ni kosa kwa mujibu wa sheria kushiriki katika shughuli za uombaji mitaani, na hivyo Serikali inawataka wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja, bila kutoa visingizio vya aina yoyote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *