
Dodoma. Serikali imetaja mkakati wa ukarabati wa meli katika Ziwa Tanganyika na kuwa mwezi ujao (Machi) ujenzi wa meli ya Mv Sangara utakuwa umekamilika.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ametoa kauli hiyo bungeni Dodoma leo Februari 14, 2025, kuwa Serikali ilishaanza mkakati wa ukarabati wa meli zinazotoa huduma katika Ziwa Tanganyika.
Kihenzile alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Bupe Mwakang’ata ambaye ameuliza Serikali ina mpango gani wa kukarabati meli katika Ziwa Tanganyika.
Amesema ukarabati wa meli ya Mv Liemba ulianza Julai 13, 2024 baada ya mkandarasi kulipwa malipo ya awali ya dola 1.9 kati ya Dola 13 milioni. zinazotakiwa kama sehemu ya malipo ya mradi mzima.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, mkataba wa mradi huo utadumu kwa kipindi cha miezi 24, hivyo unatarajia kukamilika Julai 13, 2026.
Kuhusu meli ya Mv Mwongozo, amesema mchakato wa kumpata mkandarasi wa kuikarabati meli hiyo uko katika hatua za mwisho na tayari mkandarasi M/S Songoro Marine ameshapatikana na kwa sasa taratibu za kuandaa mkataba zinaendelea.
“Mradi huo ambao utagharimu dola 4 milioni 4 umepangwa kutekelezwa ndani ya miezi sita na kuwa mradi wa meli ya MT Sangara, umefikia asilimia 98 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Machi, 2025 kwa gharama ya Dola 3 milioni,” amesema Kihenzile.
Ameongeza kuwa Serikali imetoa kipaumbele kwenye usafiri wa Ziwa hilo ambalo Tanzania inamiliki asilimia 40, hivyo haitakuwa vyema wananchi wake kuendelea kukosa usafiri.