Serikali ya DRC imesema itatuma ujumbe wake nchini Angola kwa mazungumzo yanayolenga kumaliza mzozo unaoendelea mashariki mwa nchi hiyo kati yake na waasi wa M23 wanaosaidiwa na Rwanda.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Tangazo la Kinshasa lililotolewa Jumapili jioni, limekuja siku chache kupita tangu kuwepo wasiwasi ikiwa rais Felix Tshisekedi atashiriki mazungumzo hayo au-là, kutokana na ukimya uliokuwepo baada ya tangazo la Luanda.
Mazungumzo haya yanaenda kufanyika baada ya rais Tshisekedi kuonekana kuelegeza msimamo kuhusu kufanya mazungumzo na waasi hao ambao awali aliwaita magaidi na kwamba hakuwa tayari kuzungumza nao.
Msemaji wa waasi hao, Lawrance Kanyuka kupitia ukurasa wa X wa kundi hilo, alithibitisha kupokea mwaliko wa Serikali ya Angola, bila hata hivyo kuthibitisha ikiwa watashiriki au-là, ingawa kuna uwezekano mkubwa wa wao kushiriki kwakuwa ndio wamekuwa wakishinikiza majadiliano na Kinshasa.
Nchi ya Angola imejaribu mara kadhaa kumpatanisha rais Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, hata hivyo bila mafanikio kutokana na viongozi hao kutofautiana pakubwa kuhsu namna ya kushughulikia mzozo unaoendelea, mazungumzo haya mapya yakitajwa kuwa kipimo kwa pande hizo.
Umoja wa Mataifa unasema watu zaidi ya elfu 6 wameuawa tangu mwezi Januari, huku wengine zaidi ya laki 6 wakilazimika kuhama makazi yao kutokana na mapigano mashariki mwa Congo.