Na Gideon Gregory, Dodoma
Askofu wa Kanisa la Angrikana Dayosisi ya Central Tanganyika Dkt. Dickson Chilongani amewaomba viongozi wa Serikali na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakae meza moja wamalize tofauti zao kwa njia ya mazungumzo.
Dkt. Chilongani ameyasema hayo leo Aprili 20,2025 hapa Jijini Dodoma wakati akiongoza ibada ya Misa takatifu ya Pasaka iliyofanyika katika kanisa kuu la roho mtakatifu Dodoma na kuongeza kuwa hilo ni jambo muhimu ikizingatiwa kuwa wote ni Watanzania.
“CHADEMA na CCM wote ni raia wema wa Tanzania na ni Wakristo wetu hawa, kwahiyo tuwaombe viongozi wetu wakae walimalize hili kwenye meza moja,” amesema.
Aidha, Dkt. Chilongani ameiomba Serikali iongeze jitihada katika kuondoa kero zinazowafanya Watanzania wasiwe na furaha au wawe na huzuni ambazo ni pamoja na ubadhirifu, ukilitimba na rushwa.
“Na sasa hivi mtu akienda kwenye maofisi, ofisi yoyote ile sio zote labda lakini ofisi nyingi ukiingia mtu anataka huduma, hawezi kupewa huduma mpaka aombwe uwezeshaji (facilitation), hizo ndizo kero ambazo zinawafanya watanzania wengi wasiwe na furaha ambazo zinawafanya wawe na huzuni,” ameomba.
Sambamba na hilo ametakia kila raheli timu ya Simba ambao ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa hatua ya robo faini ambapo jioni ya leo watashuka uwanjani kumenyana na Stellenbosch FC ya Afrika kusini majira ya saa 10:00 jioni katika uwanja wa Amani visiwani Zanzibar.
The post SERIKALI NA CHADEMA KAENI MEZA MOJA MMALIZE TOFAUTI ZENU – ASKOFU DKT. CHILONGANI appeared first on Mzalendo.