Serikali: Matumizi ya kondomu yamepungua Tanzania

Dodoma. Serikali imesema matumizi ya kondomu wakati wa tendo la ngono nchini yamepungua kwa kiasi kikubwa, hali inayoongeza hofu ya kuongezeka kwa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi (VVU).

Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Ziada Sellah amesema hayo jijini Dodoma leo Alhamisi Februari 13, 2025 wakati wa uzinduzi wa Siku ya Kondomu Kimataifa ambayo nchini Tanzania imefanyika kwa mara ya kwanza.

Ziada amesema utafiti inaonekana matumizi salama na sahihi ya kondomu yamepungua kwa kiasi kikubwa nchini.

“Tunapoacha kutumia kondomu tunajiweka kwenye mazingira magumu ya kuwa na ongezeko la mimba zisizotarajiwa na magonjwa mengine ya zinaa,” amesema Ziada.

Hata hivyo, taarifa za Wizara ya Afya zinaonyesha maambukizi ya VVU yamepungua kwa asilimia 2.6.

Akizindua kongamano la Kitaifa kuelekea Siku ya Ukimwi Duniani ambayo huadhimishwa Desemba mosi 2024, Waziri wa Afya, Jenister Mhagama alisema maambukizi yamepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2003/2004 hadi asilimia 4.4 kwa mwaka 2022/23.

Katika hatua nyingine, Dk Ziada amesema pia matangazo ya elimu kuhusu madhara ya Ukimwi nayo yamepungua kwa kiasi kikubwa, jambo linalopunguza hofu ya watu na kuonga ugonjwa huo si tatizo.

Mmoja wa vijana walioshiriki mdahalo huo, Everyne Uwiso amesema programu ya matumizi ya kondomu inawasahau watoto wa kike ambao ni waathirika wakubwa.

Everyne amesema kuna mashirika mengi yameibuka kusaidia kugawa kondomu bure, kwa jina la ‘Zana’ lakini zinawalenga wanaume wakati za watoto wa kike hazisambazwi hivyo.

Mwenyekiti wa waendesha bodaboda katika Soko la Machinga jijini Dodoma, Joseph Mlinga amesema vijana wengi hawapendi kutumia kondomu kwa sababu ambazo hazina msingi.

Mlinga amesema wengi wanahisi kuwa mwenye kubeba kondomu ni malaya na mara kadhaa huweza kutengwa na wenzake.