
Dodoma. Mwelekeo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/2026 imeonyesha ongezeko la asilimia 13, ikikua kutoka Sh50.29 trilioni katika mwaka wa fedha 2024/25 hadi kufikia Sh57.04 trilioni, ikiwa na vipaumbele sita.
Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25 ilikuwa Sh49.34 trilioni. Hata hivyo, Februari 14, 2025 Bunge lilipitisha bajeti ya nyongeza ya jumla ya Sh945.7 bilioni, kufuatia maombi ya Serikali yaliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na hivyo kuifanya bajeti hiyo kufikia Sh50.29 trilioni.
Dk Nchemba alisema nyongeza hiyo ililenga kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta muhimu za elimu, afya, utalii na kutoa ufadhili kwa programu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mwelekeo wa bajeti
Akiwasilisha katika Kamati ya Bunge zima Mapendekezo ya Mfumo na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26 leo March 11, 2025, Waziri Nchemba amesema kati ya fedha hizo zitakazoombwa, Sh40.9 trilioni ni mapato ya vyanzo vya ndani (asilimia 69.7), wakati Sh16.07 trilioni zitakuwa fedha za mikopo ambazo ni asilimia 30.3.
Dk Nchemba pia ametaja vipaumbele sita katika mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2025/26, ikiwamo kulipa deni la Serikali.
Ingawa hakutaja deni hilo, hadi kufikia Novemba 4, 2024 deni la Serikali lilifikia Sh96.88 trilioni ambalo lilikuwa ni ongezeko la asilimia 18.2 ukilinganisha na Sh81.98 trilioni katika kipindi kama hicho 2023.
Amesema vipaumbele vingine ni malipo ya mishahara na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Pia, vipaumbele vingine ni uimarishaji wa demokrasia, amani, utulivu na usalama, pamoja na maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
“Aidha, bajeti hii itahusisha maandalizi ya utekelezaji wa nyenzo za Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, vilevile imezingatia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya sera za washirika wa maendeleo ikiwemo Marekani,” amesema Dk Nchemba.
Sababu za ongezeko
Akizungumza ongezeko la makadilio hayo, Nchemba amesema limetokana na mikakati mbalimbali ya kiutawala na kisera inayotokana na umadhubuti katika ukusanyaji wa mapato.
Kuhusu akiba ya fedha za kigeni, Dk Nchemba amesema hadi Desemba 2024, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola 5.5 bilioni ambazo zinatosheleza uagizaji wa bidhaa kwa kipindi cha miezi 4.5.
Katika hotuba hiyo, Dk Nchemba amesema kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Januari 2025, Tanzania ilipokea Sh3.8 trilioni ambazo ni sawa na asilimia 114.3 ya lengo la Sh3.3 zilizotarajiwa.
“Kwa kipindi hicho Tanzania ilikopa Sh1.56 trilioni kutoka vyanzo vya nje kwa masharti ya kibiashara, ambayo ni asilimia 89.3 ya lengo lililokusudiwa la Sh1.75 trilioni na fedha hizo ziligharamia ujenzi wa barabara, reli, nishati, viwanja vya ndege na upatikanaji wa huduma za kijamii nchini.
Fedha zingine zilizokopwa ni Sh3.9 trilioni ambazo zilipatikana kwa soko la ndani na kati ya hizo, Sh2.3 trilioni zililipa hati fungati zilizoiva wakati Sh1.6 trilioni zilipelekwa kwenye miradi ya maendeleo.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema pato la nchi limekua huku mfumuko wa bei ukishuka hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.2 kwa kipindi kama hiki mwaka jana.
Profesa Mkumbo amesema katika bajeti ijayo ya 2025/26, Tanzania haitarajii kuanzisha miradi mipya badala yake itaendelea kutekeleza miradi inayoendelea, labda kama kuna utakaokwenda kutoa ajira kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hadi sasa jumla ya miradi 9,711 inatekelezwa nchini ikiwemo miradi kielelezo 17.
Katika hatua nyingine Profesa Mkumbo amesema Serikali imeshafanya tathmini kuhusu baadhi ya misaada inayositishwa na mataifa ya nje kwa watu wenye uhitaji wa huduma muhimu za kiafya, elimu, maji na ajira.
“Katika kukabiliana na changamoto hii, pamoja na hatua zingine, Serikali,inakusudia kuimarisha Mfuko wa Ukimwi (AIDS Trust Fund) kwa kuufanyia mabadiliko na kuongeza fedha ili kuimarisha upatikanaji wa fedha za kugharamia matibabu ya Ukimwi, TB, malaria na chanjo,” amesema.
Amesema Serikali inakusudia kuimarisha njia mbadala za kugharamia miradi kama vile kutumia njia za ubia wa sekta binafsi na sekta ya umma (PPP) ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa nchi.