Dodoma. Serikali ipo mbioni kutambulisha leseni mpya ya uzalishaji wa chumvi ili kuiondoa bidhaa hiyo katika kundi la madini mengine hivyo, kuchochea ukuaji wa tasnia ya uzalishaji chumvi nchini Tanzania.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Madini, Anthony Mavunde na uongozi wa Chama cha Wazalisha Chumvi Tanzania (Taspa), ambacho kimelenga kuboresha sekta ya madini kupitia tasnia ya chumvi.
Kwa mujibu wa Mavunde mikakati ya Serikali ni kuhakikisha sekta hiyo inapiga hatua kutokana na umuhimu wake na kuchangia sehemu ya pato la Taifa.
“Huu ni mwendelezo ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) ambaye anataka kuwawezesha wachimbaji wa madini na wazalishaji wa madini chumvi nchini, ili kuchochea ukuaji wa sekta ya madini.

“Serikali imesikia kilio chenu cha muda mrefu cha uwepo wa leseni moja ya uzalishaji wa chumvi ambayo itasaidia kumuinua mzalishaji wa chumvi kwa kupunguza gharama za uzalishaji na kuyaondoa madini chumvi katika kundi la madini mengine,” amesema Mavunde ambaye kesho Mei 2, 2025 atawasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2025/2026 bungeni mjini Dodoma.
Mavunde anawasilisha bajeti hiyo wakati ambao sekta ya madini imefikia lengo la kuchangia asilimia 10.1 ya pato la Taifa kabla hata ya kufikia mwaka 2026. Awali, ilipangwa kuwa ifikapo mwaka 2026, mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa ufikie asilimia 10.1.

Mavunde katika kuhakikisha utelekezaji huo unafanyika kwa wakati, ameelekeza mchakato wa mabadiliko ya sheria kuanza ili kuruhusu uanzishwaji wa leseni maalumu ya uzalishaji chumvi ambayo pia tozo yake kwa hekta iangaliwe upya hadi kufikia Sh20,000 kutoka kiwango kilichopo sasa.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuona wazalishaji wa chumvi wanaongeza tija na kufikia hatua ya kumiliki viwanda vya uchakataji na usafishaji chumvi nchini, ili chumvi ya Tanzania iwe yenye ubora na shindani.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahaya Samamba amepongeza kazi inayofanywa na Taspa katika kuwaendeleza na kuwasimamia wazalishaji chumvi nchini.
Amesema Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha ikiwemo kutatua changamoto za wanachama wake ili kufikia malengo.
Mwenyekiti wa Taspa, Hawa Ghasia amepongeza utaratibu wa Serikali wa kuwasikiliza wadau na kutafuta suluhisho ya changamoto zinazowakabili.

Pia, ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kusikia kilio cha wazalishaji wa chumvi kwa kujenga kiwanda cha kuchakata na kusafisha bidhaa hiyo kinachojengwa mkoani Lindi na Shirika la Madini la Taifa (Stamico).